Mauaji Tarime; LHRC wataka mgodi wa Barrick ufungwe

Nembo ya Kampuni ya Barrick ya Tanzania


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kimeitaka Serikali kufunga uzalishaji katika mgodi wa Barrick hadi hapo ufumbuzi wa kudumu utakapopatikana juu ya mgogoro uliopo.

Akizungumza jana Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Francis Kiwanga aliishauri Serikali ifanye hivyo kutokana na mauaji yaliyofanywa na polisi katika mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

Alisema LHRC inalaani vikali mauaji hayo kwani ni uchukuaji sheria mkononi jambo ambalo ni hatari kufanyika kwa vyombo vinavyolinda usalama wa watu na mali zao.

“Vyombo vya usalama na hasa Jeshi la Polisi wana wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zao, pia haki ya kuishi ni haki ya kila binadamu kama ilivyoainishwa katika katiba ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 14 ikumbukwe kuwa kukatisha uhai wa mtu ni kosa la jinai kama inavyoainishwa katika kifungu cha 196 cha sheria ya adhabu sura 16,” alisema Kiwanga.