Na James Gashumba, EANA-Arusha
NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeboresha mazingira ya biashara kwa wajasilia mali katika mataifa yao kwa kutekeleza mabadiliko muhimu ya kisheria, ripoti ya Benki ya Dunia imeonyesha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya “Kufanya Biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki 2012,” nchi tano za Jumuiya hiyo zimetekeleza kwa ujumla wao mabadiliko 10 ya kisheria kwenye biashara katika maeneo tisa yaliyopimwa.
Ripoti inaeleza kuwa kuanzisha biashara sasa ndani ya nchi za EAC zinahitajika taratibu 10 na kugharimu wastani wa asilimia 55 ya pato la kwa mwaka, ukilinganisha na taratibu 12 zilizogharimu wastani wa pato la mwaka la asilimia 140, miaka saba iliyopita (2005).
Ripoti hiyo imetayarishwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), ilitolewa rasmi Jumatano wiki hii mjini Bujumbura, Burundi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mazingira ya biashara ya wajasilia mali yameboreshwa katika kanda hiyo yenye nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda kati ya 2010 na 2011 kufuatia mabadiliko ya sheria na taratibu.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa Burundi ni miongoni mwa nchi 10 zinazoshika nafasi ya juu kabisa katika kuboresha uchumi wake duniani kati ya 2010 na 2011 ikiwa imetimiza mabadiliko ya kisheria manne, ambayo ni pamoja na shughuli za upatikanaji wa vibali vya ujenzi, kulinda haki za wawekezaji, ulipaji wa kodi na utatuzi wa migogoro ya ufilisi.
“Takwimu mpya zinaonyesha umuhimu wa upatikanaji wa taarifa za taratibu za ufanyaji biashara.Kuongezeka kwa juhudi za serikali katika kanda na ulimwenguni kwa ujumla kunatoa nafasi ya kuongezeka kwa upatikanaji wa taarifa na uwazi,” ripoti imefafanua.
Taarifa hiyo inasema, Rwanda inaendelea kushika nafasi ya kwanza katika kanda, na kwamba imefanya mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
“Duniani, Rwanda inashika nafasi ya pili kwa kujiletea maendeeleo. Katika kipindi hicho Rwanda imetekeleza mabadiliko 22, na kurahisisha ufanyaji biashara katika maeneo tisa ya mabadiliko ya kisheria,” ilifafanua ripoti hiyo.Hivi sasa inachukua masaa sita tu kusajili biashara nchini Rwanda.
“Natoa onyo kutokana na matokeo ya ripoti ya mwaka huu, naona yote mawili, yaani matunda kufanya mabadiliko ya kisheria ya ufanyaji biashara na kupungua kwa wastani wa kero za huduma hiyo,” alisema Katibu Mkuu wa EAC Dk Richard Sezibera wakati wa kutolewa rasmi kwa ripoti hiyo mjini Bujumbura.
Alitoa wito wa kuimarisha zaidi utoaji huduma bora katika biashara. Kwa wastani EAC imeshika nafasi ya 115 kati 183 katika uchumi wa dunia kwa mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo alisema kama EAC ingekumbatia utendaji bora katika utoaji huduma za biashara katika nchi zote wananchama kwa kila kiashiria cha ufanyaji bora wa biashara, kanda hiyo ingeweza kushika nafasi ya 19 duniani, sawa na Ujerumani.