Rais Kikwete aelekea Brazil kikazi

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Kikwete ameondoka jana Aprili 14, 2012, jioni kuelekea Brazil kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tano nchini humo. Katika ziara hiyo Rais Kikwete anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dilma Varna Rousseff wa Brazil na Rais mstasafu wa nchi hiyo Mheshimiwa Inacio da Silva Lula na viongozi waandamizi wa nchi hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete atahudhuria mkutano wa mwaka wa wakuu wa nchi zinazoshiriki katika Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini (Open Government Partnership-OGP) utakaofanyika mjini Brasilia chini ya Uenyekiti wa Rais Rousseff na kuhudhuriwa na wajumbe wapatao mia nne (400) kutoka serikalini, Asasi zisizo za kiserikali, Sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Kimataifa.

Ubia wa Uwazi Serikalini au kwa kifupi OGP, ni mpango uliozinduliwa Septemba 2011 mjini New York, Marekani kwa lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki katika kuamua mambo yanayowahusu, kupitia vyama visivyo vya Kiserikali na vya Kijamii.

Ubia huu unashirikisha kwa usawa wawakilishi wa serikali kwa upande mmoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali za Kijamii kwa upande mwingine. Nchi ya Brazil kwa kushirikiana na Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma ubia huu.

Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia mkutano huo tarehe 17 Aprili, asubuhi mara tu baada ya hotuba ya ufunguzi itakayotolewa na Mwenyekiti wa mkutano huo Rais Dilma Rousseff ambapo ataelezea maendeleo iliyofikia katika kuandaa mpango kazi wa kutekeleza ahadi ya kuongeza uwazi kama ilivyokubaliwa katika kikao kilichofanyika Disemba 2011. Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 20 Aprili, 2012.