RAUNDI ya 23 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 23 kesho, Aprili 14 mwaka huu kwa mechi nne. Polisi Dodoma wataikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar mjini Turiani.
Mechi nyingine za raundi hiyo zitakuwa kati ya Kagera Sugar na African Lyon zitakazooneshana kazi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Nayo Moro United inaikaribisha Oljoro JKT katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi ya 23 itakamilika Jumapili (Aprili 15 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Yanga itakuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Villa Squad itapambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 18 mwaka huu kwa mechi tano. Kagera Sugar vs Yanga mjini Bukoba, Toto Africans vs African Lyon jijini Mwanza, JKT Ruvu vs Simba- Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Ruvu Shooting vs Moro United mjini Mlandizi na Polisi Dodoma vs Coastal Union mjini Dodoma.
Wakati huo huo; timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Twiga Stars) itacheza mechi ya kirafiki na timu ya wasanii wa filamu ya Bongo Movie itakayofanyika Jumamosi (Aprili 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Lengo la mechi hiyo ya maonesho (exhibition) ni kuichangia Twiga Stars ambayo hivi sasa iko kwenye mashindano ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Pia asilimia mbili ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi ya Twiga Stars na Bongo Movie yatakwenda kwenye familia ya mwigizaji nguli wa filamu Tanzania, Stephen Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7 mwaka huu.
Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP C na B na sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu. Mechi itaanza saa 10 kamili jioni.
Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ambayo inashiriki michuano ya AWC. Wachangiaji wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389.