Tanzania ‘kukumbwa’ na Tsunami

Eneo la Pwani ya Tanzania, jijini Dar es Salaam

NCHI zilizo katika Pwani ya Bahari ya Hindi ikiwemo Tanzania zimeshauriwa kuchukua tahadhari baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.6 kutokea chini ya bahari katika ufukwe wa Jimbo la Aceh Kaskazini mwa Indonesia.
Katika pwani ya Bahari ya Hindi barani Afrika nchi zinazoshauriwa kuchukua tahadhari ni pamoja naTanzania mikoa ya Lindi na Dar es salaam,Somalia maeneo ya Cape Gauro, Hilalaya, Mogadishu, Kaamboni, nchini Kenya eneo la pwani ya Mombasa, nchini Msumbiji maeneo ya Cabo Delgado, Angoche, Quelimane,Maputo,Beira, nchini Afrika Kusini maeneo ya Prince Edward,Durban,Port Elizabeth naCape Town. Kituo cha Tahadhari cha Tsunami katika Pacific (PTWC) kimesema tsunami imetokea lakini athari zake hazijajulikana wazi bado. Inashauriwa kuwa mamlaka za nchi katika ukanda wa Bahari ya Hindi ‘zichukue hatua muhimu,’
Eneo hilo linakumbwa mara kwa mara na matetemeko ya ardhi. Tsunami ya Bahari ya Hindi ya mwaka 2004 watu 170,000 walikufa Aceh.
Afisa mmoja alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema sentimeta 17 (inchi 6.7) za tsunami zimetokea na mitetemo yake ilikuwa inaelekea katika pwani ya Aceh. Utafiti wa Kituo cha Utafiti cha Marekani (USGS) kinachoweka kumbukumbu za matetemeko ya ardhi duniani kote, kilisema kuwa tetemeko la Aceh lilikuwa kwenye mzunguko wa kilometa 33 (maili 20) chini ya bahari karibu kilometa 495 kutoka Banda Aceh makao makuu ya jimbo.
Awali kulikuwa na ripoti za tetemeko kuwa na ukubwa wa 8.9 lakini ikapitiwa upya na kituo cha USGS kufikia 8.6. Kisha kukawa na ripoti za mitetemo baada ya tetemeko hilo kubwa. Inadaiwa kuwa kumekuwa na taarifa za ardhi kutetemeka kwa muda wa mpaka dakika tano.
Kituo cha PTWC cha tahadhari kilisema kuwa matetemeko ya aina hiyo yenye ukubwa huo “yana uwezekano wa kufikiwa na uharibifu unaosambaa wa tsunami ambao unaweza kuathiri eneo lote la pwani ya Bahari ya Hindi katika ukanda wake “.
Tahadhari nyingine ilisema vipimo vya kiwango cha bahari kinaonyesha kuwa kunaweza kuwa na mitetemo ya tsunami, hii “inaweza kuleta uharibifu sehemu kadhaa za pwani “.
Rais wa Indonesia Susilo Bambang Yudhoyono ameviambia vyombo vya habari katika mji mkuu wa nchi hiyo kuwa hakujawa na taarifa za Tsunami lakini ‘tunachukua tahadhari” Alisema, ‘Mtandao wetu wa tahadhari unafanya kazi vizuri na nimeamuru timu ya maafa na misaada kwenda kwa ndege mara moja Aceh kuhakikisha kuwa hali inadhibitiwa na kuchukua hatua zozote muhimu zinazotakiwa’ alisema. Bruce Presgrave wa kituo cha Marekani USGS ameiambia BBC kuwa tetemeko hilo lilisababishwa na ardhi kwenda mlalo zaidi kuliko wima kwa hiyo halijasababisha maji mengi kuhamishwa.
-BBC