Madaktari wachunguza mwili wa Kanumba

Steve Kanumba

Jopo la madaktari jana lilianza kuuchunguza mwili wa aliyekuwa mcheza filamu maarufu nchini, Steven Kanumba, kwa lengo la kubaini sababu zilizosababisha kifo chake kilichotokea Jumamosi iliyopita majira ya alfajiri jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema taarifa kuhusiana na uchunguzi huo itatolewa na madaktari baada ya kuukamilisha.

“Leo (jana), madaktari wapo kwenye ukaguzi maalum ambao taarifa yao itakuwa ni moja ya ushahidi wa kitaalam utakaobaini sababu za kifo cha msanii huyo, ” alisema Kamanda Kenyela.

Aliongeza kuwa uchunguzi uliofanywa na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) unatarajiwa kuwekwa wazi leo.

Alisema katika uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi limebaini kuwa wivu wa kimapenzi ndiyo uliosababisha ugomvi kati ya Kanumba na Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu.

Kamanda Kenyela alifafanua kuwa ugomvi huo ulizuka baada ya Lulu kupigiwa simu na mtu ambaye bado hajajulikana na marehemu Kanumba, kutaka kumfahamu mtu huyo aliyempigia.

Alisema mbali na Jeshi hilo kuzishikilia simu za marehemu Kanumba na Lulu, kwa uchunguzi zaidi wa mawasiliano hayo, pia linaendelea na kuvifanyia uchunguzi vielelezo vingine ambavyo vilikuwamo ndani ya chumba cha Kanumba.

Miongoni mwa vielelezo hivyo ni pombe kali aina ya vodka, panga na soda aina ya sprite.

Aidha, Kamanda Kenyela alisema Jeshi hilo linaendela kumshikilia Lulu, huku taratibu za kisheria zikiendelea kufuatwa na kuongeza kwamba taratibu zikikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Aliwataka mashabiki wa msanii huyo kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Polisi walimkamata Lulu tangu Jumamosi iliyopita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo kwa kuwa ndiye aliyekuwepo chumbani kwa marehemu.

CHANZO: NIPASHE