MAKAMU wa Rais wa Malawi Joyce Banda ameapishwa kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia kifo cha Bingu wa Mutharika. Banda anakuwa rais wa kwanza wa kike kusini mwa Jangwa la Sahara, na aliapishwa mbele ya bunge katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe.
Taarifa zinasema Bi. Banda, ambaye alikuwa makamu wa rais tangu mwaka 2009, alishangiliwa na kupigiwa kofi kabla na baada ya shughuli hiyo. Mutharika, 78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alhamis, ingawa kifo chake hakikuthibitishwa hadi Jumamosi.
Kuchelewa kutangazwa kifo chake kulisababisha wasiwasi kuhusu nani anaongoza nchi hiyo.
Kulikuwa na tetesi kuwa watu wa karibu wa rais Mutharika walikuwa wakitaka kubadili katiba ya nchi ili kuzuia Bi Banda kuchukua madaraka, na badala yake kumpa ndugu yake, Peter Mutharika ambaye ni waziri wa mambo ya nje.
Bi Banda alifarakana na rais Mutharika mwaka 2010 na kuwa mkosoaji mkubwa wa rais. Alifukuzwa kutoka chama cha DPP na kuunda chama chake cha Peoples Party.