Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF- kuomboleza kifo cha msanii maarufu nchini Steven Charles Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia Aprili 7, 2012.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amemwomba kiongozi huyo wa TAFF kufikisha salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba na kwa wasaani wote nchini ambao wamepotelewa na mdau na mwenzi wao.
Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye amemwelezea kuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye katika uhai wa maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema Rais: ”Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya filamu nchini hautasahaulika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ndugu Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu ya Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi yetu.”
“Nakutumia wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa. Aidha, naomba unifikishie salamu za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa.
Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa sababu yote mapenzi yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote nchini kuwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba. Amen.”