Rais Kikwete atuma rambirambi Malawi

Bingu Wa Mutharika

Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Makamu wa Rais wa Malawi, Joyce Banda kuomboleza kifo cha kiongozi wa nchi hiyo, Rais Bingu wa Mutharika.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemwambia Banda kuwa Tanzania imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Rais Bingu wa Mutharika ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama kiongozi wa karibu na rafiki mkubwa wa Tanzania.
Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo, “Sisi katika Tanzania tumepokea taarifa za kifo cha Rais Bingu wa Mutharika kwa mshtuko na majonzi. Alikuwa kiongozi na rafiki wa karibu wa Tanzania na rafiki yangu. Alikuwa kiongozi wa kutumainiwa miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika lote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa hakika, Afrika imempoteza kiongozi imara, aliyeamini katika maslahi ya Bara letu na watu wake. Siku zote tutamkumbuka kwa dhamira yake na moyo wake katika kupigania umoja, amani, utulivu na ustawi wa mataifa yetu mawili na Afrika nzima.”
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Mheshimiwa, familia ya marehemu na wananchi wote wa Malawi salamu za rambirambi za dhati ya mioyo yetu kufuatia kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Rais Bingu wa Mutharika,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake.