Na Mwandishi Wetu
MSANII maarufu wa sanaa ya kuigiza nchini Tanzania, Steven Kanumba amefariki dunia. Taarifa zinasema Kanumba amefariki dunia usiku wa kuamkia leo alipokuwa nyumbani kwake Sinza-Vatcan jijini Dar es Salaam.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa na Jeshi la Polisi zinasema Kanumba amefariki dunia baada ya kusukumwa katika ugomvi na mtu anayedaiwa kuwa mpenzi wake walipokuwa wakizozana nyumbani kwake.
Binti huyo aliyetambulika kwa jina moja la ‘Lulu’ anadaiwa kumsukuma Kanumba kisha akaanguka chini na kugonga kichwa kwenye sakafu, kitendo kinachohofia ndicho kilichosababisha kifo chake. Tayari polisi Dar es Salaam imethibitisha kifo cha staa huyo wa tasnia ya uigizaji japokuwa hawajasema nini kilichosababisha kifo chake.
Maiti ya Kanumba kwa sasa imeifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ukisubiri uchunguzi wa madaktari na kisha taratibu za mazishi kufanyika. Mtandao huu mmezungumza na mmoja wa watu wa karibu wa msanii huyo na kudai hivi sasa kuna umati mkubwa nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam na taratibu za mazishi zinafanywa. Tutaendelea kuwapa taarifa zaidi juu ya tukio hili mara baada ya kuzipata.
Uongozi na wasomaji wa mtandao huu unatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa msanii huyo. Amina.