Tenga alaani mauaji ya Mohamed Nur Somalia

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amepokea kwa masikitiko taarifa za shambulizi la kigaidi lililofanywa Aprili 4 mwaka huu jijini Mogadishu, Somalia na kupoteza maisha ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Somalia (SFF), Said Mohamed Nur.

Kwa niaba ya TFF na wadau wa mpira wa miguu Tanzania anatuma salamu za rambirambi kwa Makamu Mwenyekiti wa SFF, Ali Said Ghuled kutokana na kifo hicho cha ghafla cha shambulizi la bomu cha Nur ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Amesema Nur alishiriki kikamilifu katika kujenga maisha ya wananchi wa Somalia kwa kupitia mpira wa miguu, hivyo analaani kwa nguvu vitendo vya kigaidi ambavyo pia vimepoteza maisha ya watu wengine katika tukio hilo.

Kwa kipindi chote cha maisha yake, Nur ameutumikia mpira wa miguu katika ngazi tofauti nchini kwake na ukanda huu wa CECAFA, hivyo kifo chake ni pigo kwa Tanzania, na daima itaendelea kukumbuka mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu.

Rais Tenga amesema TFF iko pamoja na familia ya Marehemu katika kuomboleza msiba huu mzito na kuwataka wawe na uvumilivu na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa kwao.

Kwa mechi zote za TFF zitakazochezwa katika kipindi cha siku 7 zijazo kutakuwa na dakika moja ya kusimama kimya kwa ajili ya kuomboleza msiba huo. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amina.

Wakati huo huo, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Simba kesho (Aprili 6 mwaka huu) wanapambana na ES Setif katika mchezo wa marudiano wa kombe hilo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaitakiwa kila la kheri Simba kwenye mechi hiyo kwani ina uwezo wa kupata matokeo mazuri yatakayoivusha katika raundi inayofuata. Msafara wa Simba unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Dk. Sylvester Faya.

Mechi hiyo namba 46 itachezeshwa na waamuzi Ben Hassan Mohamed, Hmila Anouar, Ben Abdelmoumen Kamel na Kordi Med Said, wote kutoka Tunisia. Kamishna atakuwa Jean Fidele Diramba kutoka Gabon.