Na Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com, Arusha
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo imempoka nafasi ya ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kile ilichodai kuwa alikiuka maadili ya uchaguzi.
Uamuzi huo umetokana na hukumu ya kesi namba 13/2010 ya kupinga matokeo ya mbunge Lema iliyokuwa ikiendelea mahakamani hapo, baada ya kufunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaani Musa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel.
Katika malalamiko yao yaliosikilizwa na Jaji Gabriel Rwakibarila, wanachama hao walidai Lema alikiuka kanuni, maadili, taratibu na sheria za uchaguzi, kwa kutoa maneno ambayo yalimdhalilisha mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian.
Walalamikaji walidai Lema alitoa lugha za kashfa na udhalilishaji
wa kijinsia pamoja na kumtusi mgombea Dk. Burian kwenye kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi wa mwaka 2010.
Akitoa hukumu Jaji Rwakibarila alisema vielelezo vimeonesha kati ya mikutano 60 ya kampeni aliyoifanya Lema katika uchaguzi huo, mikutano nane imebainika kuwa alikiuka maadili ya kampeni za uchaguzi. Ameongeza kwa kuzingatia ushahidi huo Mahakama imetengua matokeo ya ubunge wa Lema baada ya kuridhika na ushahidi uliyowasilishwa.
Alisema kati ya vielelezo nane vilivyowasilishwa na walalamikaji kila kimoja, katika hoja kinanguvu ya kutengua matokeo ya uchaguzi huo. Alizitaja baadhi ya hoja kuwa ni pamoja na udhalilishaji, kutumia lugha ya matusi na lugha ya kashfa dhidi ya mgombea wa CCM, mambo ambayo ni kinyume cha maadili ya kampeni za uchaguzi.
“…Mahakama imeridhika kuwa Lema alikiuka sheria na vifungu vyake
vinavyokataza kufanya kampeni kwa misingi ya ubaguzi wa kidini, ujinsia
na kikabila, hivyo kwa misingi hiyo matokeo ya uchaguzi wa ubunge wake yametenguliwa kama walivyokuwa wameomba wadai,” alisema Jaji.
Akizungumzia madai ya udini Jaji huyo alisema kuwa Mahakama haijaridhika na ushahidi uliotolewa kwani hawajaweza kuthibitisha madai ya kuwa wanawake wanaovaa vilemba ni Al Qaeda. Mbali na mahakama hiyo kubatilisha matokeo hayo pia imemuamuru Lema kulipa gharama zote zilizotumika kuendesha kesi hiyo.
Jaji huyo pia alimwamuru Msajili wa Mahakama Kanda ya Arusha, George
Hebert kupeleka nakala ya hukumu ya kesi hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa hatua inayofuata.
Kwa upande wake Lema ametamka wazi kutoridhishwa na hukumu hiyo kwa madai kuna dosari nyingi ambazo hazikuzingatiwa.
“Ninawaomba wananchi wa Arusha msiogope, mtulie kwani sitaogopa
nilichaguliwa na nguvu za Mungu na hii kwangu ni chachu na huu ni
mwanzo wa mapambano,” alisema.
Alidai kuwa inaonesha wazi uhuru wa Mahakama haupo kwa sasa na kazi inafanywa chini ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na mahali pekee ambapo wananchi watakimbilia baada ya kukosa haki katika vyombo vya sheria ni kwenda msituni.
“Mimi niko imara na ninaweza kusihi maisha ya aina yoyote, kwani ubunge ni sehemu ya kupigania watu,nimehukumiwa kwa makosa ya uongo ni kesi ya kashfa ila hata anayedaiwa nilimkashfu hakufika mahakamani kutoa ushahidi, hii ni Hasira ya Rais Jakaya Kikwete kwani miaka mitatu iliyopita alinitaka nigombee ubunge kwa tiketi ya (CCM) ila nikakataa na pia ni hasira ya Waziri Mkuu kwa kumwita mwongo Bungeni.
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freemana Mbowe alipozungumza na wafuasi wa Chama hicho alisema Jumamosi chama hicho kitafanya mkutano wa hadhara na kutoa maamuzi ya nini kifanyike. Mbowe alisema kuwa wanafanya mawasiliano na viongozi wengine wa Chama hicho, wanasheria wa wake, juu ya namna walivyoipokea hukumu hiyo na namna walivyolitafsiri suala hilo.
“Tunahitaji mashauriano zaidi na kupitia hukumu ile na tunahitaji muda
zaidi wa kutafakari na kujua hatua zinazofuata, japo kuna haki ya
kukata rufaa au uchaguzi kurudiwa, tunataka kuangalia suala hili kwanza
kwa ukamilifu,”
“Lema amebanwa na kifungu chini ya sheria ya uchaguzi ambavyo ukihukumiwa katika makosa yanayoangukia chini ya kifungu hicho “illegal practice” kinyume cha maadili, huruhusiwi kugombea ndani ya miaka mitano hivyo tunakaa na wanasheria kuangalia hukumu hiyo na kama sheria hiyo itambana Lema kama haitambana, atagombea tena,” alisisitiza Mbowe.
Aidha aliongeza kutokana na hilo maamuzi ya chama yatatolewa Jumamosi na kutolea mfano wa kesi ya rushwa ya mwaka 1985 iliyokuwa ikimkabili waziri wa nchi, ofisi ya rais (mahusiano) Stephen Wassira ambaye alibanwa na sheria na kunyimwa kugombea kwa kipindi cha miaka mitano.
“Watu wenye mamlaka wasome alama za nyakati kwani hizi siyo enzi za mahakama kumhukumu mtu hata kama hajatenda kosa, sipendi nchi yetu ifikie yaliyoikumba Tunisia na ninasihi busara zaidi ziwe zinatumiaka katika nguvu za dola…Hukumu ya kesi hii ilivuja na kama vyombo vya dola vitaendelea kutekeleza mambo bila kufuata kanuni na sheria basin chi itachafuka,” alimalizia.