Na James Gashumba, EANA
KILA inapotokea opereshini ya kijeshi inayohusisha matumizi ya silaha, maafisa wote wa jeshi katika nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hawana budi kutumia weledi wao kisheria katika kushugulikia mgogoro wa aina hiyo, afisa mmoja mwandamzi wa jeshi la Rwanda amesema.
‘’Kama mataifa yaliyostarabika hatuna budi kila wakati kuzuia maafa yasiyo ya lazima na uharibifu katika operesheni za aina hiyo,’’ amesema Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Jenerali Charles Kayonga alipofunga mafunzo ya kijeshi ya wiki tatu juu ya maadili na sheria za kushughulikia migogoro yenye matumizi ya silaha kwa mafisa 30 wa jeshi toka nchi za EAC mwishoni mwa wiki.
Alisema: ‘’Sehemu moja inaweza isijali kuhusu maafa kwa binadamu, hususan ni kwa kupoteza maisha ya binadamu wasio na hatia kama vile ilivyotokea katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.’’
Aliwataka maafisa jeshi kuwa madhubuti na kutenda kazi kwa ufanisi katika operesheni za iana hiyo ili kuweza kukabiliana na changamaoto mpya za uhalifu kama vile ugaidi kupitia mitandao ya mawasiliano.
Hata katika operesheni za kulinda amani ambako ama raia au walinda amani wanaweza kujikuta wanashambiliwa, sheria katika hali kama hiyo pia hazina budi kuheshimiwa.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Kijeshi cha Nyakinama nchini Rwanda, yaliendeshwa na Brigadia Carl Erdlingher na Dk. Van Baardar kutoka Chuo cha Kijeshi cha Dutch Defence Academy, nchini Ujerumani.
Washiriki walibadilishana uzoefu wao katika medani ya kijeshi, vita visivyotarajiwa na changamaote za sheria za kijeshi nyakati za migogoro inayotumia silaha.