Na Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com-Moshi
MADEREVA na watumiaji wengine wa barabara mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuepuka ulevi, hatua ambayo itasaidia kupunguza matukio ya ajali ambayo yamekuwa yakiwagharimu Watanzania wengi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjro (RTO), Peter Sima, alipokuwa akitoa salamu za Siku Kuu ya Pasaka, ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha mambo ya msingi watumiaji wa barabara kwa jumla.
Amesema kipindi cha Siku Kuu (Pasaka) ni vema madereva na wadau wengine wa barabara wakabadilika na kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuzi za usalama barabarani.
“Madereva na watumiaji wengine wa barabara wakiwemo watembea kwa miguu wanatakiwa kafuata sheria na kuepuka ulevi ikiwa ni pamoja na kuwa makini pindi wawapo barabarani kwani kwa kufanya hivyo tutapunguza matukio ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikisababisha wengi kupoteza maisha huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu,” alisema Sima.
Ameongeza kuwa dereva yeyote ambaye atakiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwa mlevi, kukimbiza gari au pikipiki na nyinginezo atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kuonewa huruma. Sima aliwataka pia abiria kuacha tabia ya kushabikia mwendo kasi kutokana na kwamba hali hiyo ni kinyume cha sheria na kanuni za usalama barabarani na husababisha ajali.
Alisema ni vema pia abiria wakatoa taarifa za madereva ambao wataonekana kukiuka sheria za usalama barabarani ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kupunguza matukio ya ajali za barabarani.
Aidha alisema jeshi la polisi litaendelea na mkakati wake wa utoaji elimu ya usalama barabarani ili kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani zinafahamika vema na kufuatwa. Alisema pia wataendelea kuendesha misako ya kuwadhibiti wanaokiuka sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuhakikisha watumiaji wote wa barabara wanakuwa makini pindi wawapo barabarani.