Mifarakano kwenye ndoa huchangia watoto mitaani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba

Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com-Moshi

LICHA ya Serikali na mashirika anuai kujitahidi kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani juhudi hizo zinaonekana kugonga ukuta baada ya mkoani Kilimanjaro kubainika ongezeko hilo huchangiwa na migogoro ya ndoa ndani ya familia.

Taarifa zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwmwezi Septemba hadi Desemba 2011 jumla ya ndoa 812 ziliripotiwa kufarakana hali inayosababisha watoto kushindwa kumudu maisha ndani ya familia na kukimbilia mitaani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Agness Urassa alioitoa hivi karibuni hali ya mafarakano ndani ya ndoa imekuwa ikichangia watoto kukimbilia mitaani.

Alisema katika kipindi hicho cha miezi mitatu malalamiko yanayohusu migogoro ya ndoa yaliongezeka kutoa 698 kipindi cha mwezi Juni hadi Septemba 2011 hadi kufikia 812 katika kipindi hicho cha mwezi septemba hadi disemba.

Anaongeza kuwa malalamiko ya migogoro ya ndoa wanayopokea ni pamoja na unyumba, baadhi ya wazazi kulalamikia kutotunzwa sanjari na mimba nje ya ndoa ambapo zimekuwa zikisababisha kuzaliwa kwa watoto wasiotarajiwa na kupelekea kuzuka kwa migogoro baina ya wazazi hao wawili jambo linalofanya watoto kukosa malezi na kuishi katika maisha hatarishi. Bi. Urassa alichanganua kuwa katika malalamiko hayo 812 yalikuwa yanayolalamikia matunzo 145, Unyumba 126 na nyumba nje ya Ndoa 541.

“Migogoro ya ndoa kwa sasa imekuwa tishio na sababu kuu ya watoto kuzidi kuongezeka mitaani kwani katika ofisi yetu kesi zinazolalamikia ndoa ni nyingi na zinazidi kuongezeka, na jambo hili linakwamisha jitihada za Serikali za kutaka kupunguza wimbi la watoto hao mitaani, na hili litafanikiwa kama kila familia itajipanga upya na kutambua nini maana ya malezi na maana ya ndoa na kuondokana na mafarakano ya mara kwa mara yanayoweza kuzuilika,” alisema Bi. Urassa.

Aidha Bi. Urassa alisema hali hiyo ya migogoro ndani ya ndoa inachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ulevi wa kupindukia sanjari na baadhi ya wanandoa kushindwa kutulia ndani ya ndoa zao na kujikuta wakizaa watoto nje ya ndoa hali inayosababisha mafarakano ndani ya familia.

Alisema ili kuweza kumaliza tatizo hilo serikali inapaswa kuandaa mikakati ya utoaji elimu katika jamii hatua ambayo itasaidia kupungua kwa matatizo hayo ambayo mengi yanachangiwa na kutokuwepo kwa uelewa wa ndoa na malezi ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria ndogondogo kuanzia ngazi za vijiji za kudhibiti matatizo hayo.
Alisema pamoja na serikali kutoa elimu taasisi za dini pia zinapaswa kuongeza nguvu katika katika kukemea migogoro katika ndoa na kondokana na mtazamo kuwa kazi ya dini ni kufungisha ndoa na baada ya hapo zimemaliza kazi.

Bi. Urassa aliitaka jamii kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inapunguza ongezeko la watoto wa mitaani na kuondokana na migogoro ndani ya ndoa kwa madai kuwa jamii ikilisimamia hilo na kulitilia msisitizo tatizo hilo litapungua kama sio kuisha kabisa kutokana na kwamba jamii ndio wahusika wa watoto hao.