MALI inaweza kuwekewa vikwazo hii leo, baada ya viongozi wa kijeshi kutoonesha ishara zozote kuheshimu ahadi walizotoa za kurejesha utawala wa kiraia nchini humo.
Muda wa saa 72 uliowekwa na Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi-ECOWAS, ili wanajeshi warejee kambini umemalizika saa sita usiku, jana kuamkia leo. Viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wanakutana Dakar leo kuzungumzia hali nchini Mali, pembezoni mwa sherehe za kuapishwa rais mpya wa Senegal Macky Sall.
Kiongozi wa mapinduzi ya Mali, kapteni Amadou Sanogo, ameahidi jana kurejesha katiba na taasisi zote za taifa kabla ya kuitishwa uchaguzi. Jumuia ya ECOWAS iliyotishia kuifunga mipaka na Mali, kusitisha shughuli za kibiashara, kuitenga nchi hiyo kidiplomasia na kuzuwia akiba ya nchi hiyo katika benki kuu ya nchi za Afrika magharibi, haikujibu tangazo la Sanogo.
Rais Alassane Ouattara wa Côte d’Ivoire, Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, amesema amezungumza jana na kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Mali, kumshukuru kwa uamuzi huo, lakini hakusema kama vikwazo vitatekelezwa. Amesema atashirikiana haraka na viongozi wengine ili kuhakikisha katiba ina heshimiwa nchini Mali.
Utawala wa kijeshi umedhoofika nchini Mali. Waasi wa Tuareg wanaopigania ukombozi wa taifa lao wanaloliita Azawad-wanadhibiti miji yote mitatu ya kaskazini. Baada ya kuiteka Kidal, na Gao, jana waasi hao wameuteka mji wa kihistoria wa Timbuktu na kupandisha bendera yao.
“Waaasi wameingia katika hoteli, wamevunja kasha ya fedha. Wameuteka mji wote na kuharibu kila kitu. Watu wote wameingiwa na wasi wasi huku. Wameshaanza kuvunja benki na kuiba magari. Hakuna anaesubutu kutoka nje. Watu wote wamejifungia majumbani mwao. “wanasema wakaazi wa Timbuktu
Kanali El Hadj Ag Gamou, afisa pekee wa ngazi ya juu kutoka kabila la Tuareg, katika jeshi la Mali ametangaza kujiunga na waasi hao. Wakati huo huo Ufaransa imewataka raia wake waihame “kwa muda” Mali.
-DW