CHADEMA washinda ubunge Arumeru Mashariki

Mgombea wa CHADEMA, Nassari Joshua akitambulishwa na Dk. Wilbload Slaa katika moja ya mikutano ya kampeni zao

*CUF nao washinda Udiwani Tanga

Na Mwandishi Wetu, Arumeru

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya mgombea wake, Nasari Joshua kupata kura 32,972 na kumshinda mpinzani wake wa karibu Sumari Sioi Solomoni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 26,757.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa muda huu na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Bw. Kagenzi; amesema Joshua ameshinda baada ya kupata kura nyingi zaidi kutoka vituo 327 vilivyotumika katika uchaguzi huo.

Joshua Nassari wa CHADEMA akiwa na Nyerere katika eneo la Kikatiti


Alisema jumla ya kura halali zilizopigwa ni 60,038 huku kura 611 zikikataliwa. Akitangaza matokeo hayo alisema Mazengo Adam wa chama cha AFP amepata kura 139, Charles Msuya wa UPDP amepata kura 18 huku mgombea Chipaka A Moova wa TLP akiambulia kura 18.

Amesema mgombea Kirita Shaurimoyo wa SAU amepata kura 22, Hamis Kiemi wa chama cha NRA kura 35, Mohamad Mohamad wa chama cha DP amepata kura 77, huku Sioi Solomoni wa CCM akijivunia kura 26,757.

Taarifa ambazo pia mtandao huu umezipata kutoka mkoani Tanga CCM imeshindwa katika uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Msambweni Tanga mjini. Kata hiyo imechukuliwa tena na Chama cha Wananchi CUF baada ya kufanyika uchaguzi kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo kutoka Chama cha CUF kufariki dunia hivi karibuni.