Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Watoto (TAJOC) kimesajiliwa rasmi juzi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Akizungumza baada ya kupata usajili huo jijini Dar es Salaam jana, Mweyekiti wa TAJOC, Rosemary Mirondo, alisema kusajiliwa kwa chama hicho ni mafanikio kwa waandishi wa habari katika kupigania haki za watoto.
Mirondo alisema kuwa malengo ya chama ni kuhakikisha watoto wanatetewa katika kupata haki zao za msingi pamoja na kupinga ajira za utotoni.
“Tunategemea kufanya kazi kwa karibu na wadau wengine katika kupata ushauri katika kupata habari za watoto na kufikisha kwa watunga sera kuhakikisha watoto wanapewa haki zao,” alisema Mirondo.
Alisema kuwa chama kina wanachama 50 ambao wanatoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini, ambao watakuwa wanajikita katika kupata habari zinazohusu watoto kupata haki zao.
Mirondo alisema pamoja na mambo mengine chama hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi katika kuweza kuwafikia watoto lakini ana imani kwamba kwa kushirikiana na wadau suala hilo litaweza kufanikiwa.
Alieleza kwamba wanachama hao wanahitaji kujengewa uwezo wa kutosha katika kutoa taarifa za watoto kwa kulinda haki zao katika vyombo vya habari nchini, hivyo aliwaomba wadau kujitoa ili kuwawezesha.