Serikali yasema itaendelea kuliboresha Jeshi la Polisi

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP, Said Mwema

Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi-Moshi

SERIKALI imesema itaendelea kuliboresha Jeshi la Polisi nchini ili liweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali. Hayo yamebainishwa leo mjini Moshi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbara Abduluwakuili wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa askari wapya wa Jeshi la Polisi yaliyokuwa yakifanyika kwenye Chuo cha Taaluma ya Jeshi la Polisi Moshi (Moshi Police Academy).

Abduluwakili amesema kutokana na mabadiliko ya Kisayansi, hali ya uhalifu imekuwa ikibadilika kimazingira na hivyo aina na mbinu za uhalifu nazo zimebadilika hali ambayo inalilazimu Jeshi la Polisi nalo libadilike kimbinu kwa kujiongezea ujuzi ili kukabiliana na wahalifu kikamilifu.

Amesema pamoja na changamoto hizo, hivi karibuni, Jeshi la Polisi limeweza kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali hasa kwenye suala la kupambana na wahalifu wakiwemo wakorofi na wale wanaotumia silaha za moto na hata kuwashinda na kuwatia nguvuni.

Ameongeza kuwa hivi sasa hata takwimu za makosa ya Jinai yanayoripotiwa katika vituo mbalimbali vya Polisi yamepungua hali inayoonyesha kuwa hali ya uhalifu nayo imepungua kwa kiasi kikubwa. Amepongeza juhudi zinazofanywa na makamanda wa Polisi wa Mikoa chini ya Uongozi wa Mkuu wa Jeshi hilo Inspekta Jenerali Saidi Mwema katika kuhakikisha kuwa hali inazidi kuwa salama na utuliu kuongezeka siku hadi siku.

Kuhuusiana na ajali za barabarani, Abdulwakili, amewata Polisi kuhakikisha kuwa wanaendeleza juhudi zao za kupambana na madereva wakorofi na hata ikiwezekana kuwanyang’anya leseni kwa madereva na kuyaondoa barabarani magari mabovu ili kuepusha ongezeko la ajali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, amesema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki na chaguzi nyingine ndogondogo kwa nafasi za udiwani hapa nchini zinafanyika kwa amani na utulivu.

Amewataka wananchi waliopo kwenye maeneo ya upigaji kura waweze kupiga kura zao na kurudi majumbani kusubiri matokeo na kuepuka kufanya vurugu kwani kwa kufanya hivyo watalilazimisha Jeshi la Poilisi kuwachukulia hatua za kisheria.

Akizungumzia kazi inayowakabili askari hao wapya, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Saidi Mwema amesema kuwa kazi ya Polisi ni kuhakikisha kuwa inapambana na changamoto mbalimbali na amewataka kuzigeuza changamoto hizo ili ziwe ni fursa ya kutumia rasilimali chache zilizopo kwa kuleta mafaniko ya kiutendaji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Awali akitoa taarifa ya Mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi cha Moshi ACP Matanga Mbushi, amesema kuwa pamoja na mambo mengine, wahiitimu hao wamejifunza kazi za Polisi, utoaji wa huduma bora kwa mteja anayefika katika kituo cha Polisi, Polisi Jamii na sheria mbalimbali za kitaifa na za Kimataifa. Jumla ya Askari Polisi 3264 wakiwemo wanaume 2373 na wanawake 891wamehitimu mafunzo yao ya awali ya miezi sita na kupangiwa kazi katika mikoa mbalimbali.

Sherehe hizo ambazo pia zilihudhuliwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa na Wakuu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Wakuu wa Vyuo vya Polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji na wananchi, zilitanguliwa na Mgeni Rasmi kukagua gwaride na kutoa zawadi kwa askari 12 waliofanya vizuri zaidi ya wengine kabla ya kuona maonyesho ya Ujasiri na utayari wa wahitimu.