Wanafunzi Mahinda sekondari ‘wauza’ bangi

Misokoto ya bangi

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WAKAZI wanaoishi maeneo ya kuzunguka Shule ya Sekondari Mahida iliyoko wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wamelalamikia vitendo vinavyofanywa na wanafunzi wa shule hiyo ikiwemo uuzaji wa bangi, ujambazi mitaani na ngono zembe hali ambayo imesababisha ongezeko la mimba katika shule hiyo na kushuka kwa kiwango cha taaluma.

Wakazi hao wakiwemo wazazi wa watoto katika shule hiyo pia wameutupia lawama uongozi wa shule hiyo kushindwa kusimamia suala la nidhamu hivyo kusababisha wanafunzi kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo uuzaji wa madawa ya kulevya na ujambazi vitendo ambavyo hufanywa na watoto wa kike.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa shule hiyo jumla ya
wanafunzi saba wa kidato cha nne mwaka huu wamebainika ku ujauzito hali ambayo imeelezewa kuchangiwa na kushuka kwa nidhamu katika shule hiyo na kusababisha shule hiyo kupata matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Wakizungumzia suala hilo kwenye kikao cha wazazi kilichoitishwa na uongozi wa shule hiyo baadhi ya wazazi walisema uongozi wa shule hiyo umeshidwa kusimamia nidhamu miongoni mwa wanafunzi ikiwemo suala zima la taamuma shuleni hapo hivyo kusababisha vitendo viovu kuendelea kushika kasi.

“Wanafunzi katika shule hii wamekuwa na vitendo vichafu sana kwani wamekuwa wakijihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo huuzwa na wasichana pamoja na kufanya vitendo vya ujambazi mitaani hivi ni vetendo vya aibu sana ambavyo vimekuwa vikisababisha matokeo mabaya katika shule hii,” alisema mmoja wa wazazi hao.

Akizungumza, Baltazary Morisi mmoja wa wazazi wa wanafunzi shuleni hapo alisema suala la uuzaji wa bangi katika shule hiyo limesababisha madhara makubwa ikiwemo kuchangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya Ngono zembe na kuporomoka kwa taaluma.

Aidha alisema vitendo ambavyo vimekuwa vikifanywa na wanafunzi hao shuleni na mitaani ni vya aibu na vya kusikitisha hivyo walimu wangepaswa kudhibiti vitendo hivyo na kwamba bhangi hiyo wamekuwa wakiiuzia shuleni na si nyumbai ambapo wataonekana na wazazi.

“Walimu katika shule hii wanapaswa kusimamia kikamilifu suala la nidhamu na kuhakikisha wanakomesha vitendo vyote viovu ikiwemo vya uvutaji wa madawa ya kulevya, ujambazi na hata ngono zembe ambazo zimekuwa zikisababisha wanafunzi kupata ujauzito,” alisema.

Akizungumzia malalamiko hayo mkuu wa shule hiyo, Henry Masawe alikiri kuwepo kwa wanafunzi saba waliobainika kuwa na ujauzito na kusema kuwa mwalimu si wakulaumiwa kutokana na vitendo viovu vya wanafunzi kutokana na kwamba wazazi ndio wanaopaswa kusimamia maadili ya watoto wao na kuhakikisha wanazingatia masomo.

Alisema kazi ya mwalimu ni kusimamia nidhamu ya mwanafunzi pindi awapo shuleni lakini akishatoka ni jukumu la mzazi hivyo kama kuna wanafunzi ambao wanajihusisha na vitendo vya kijambazi mitaani mzazi ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kushindwa kumlea mtoto wake na si walimu.

“Wazazi ndio wanaishi na watoto wao majumbani na wanapaswa kufuatilia vema maadili ya watoto wao wawapo nyumbani, shuleni na hata mitaani, lakini wanapotupa lawama kwa walimu eti wameshindwa kusimamia nidhamu hili si sahihi kabisa kwani wao ndio wangepaswa kuwa mstari wa mbele katika kukemea maovu kwa watoto wao,” alisema Masawe.