Rais Kikwete atuma rambirambi kwa familia ya Balozi Haji Lukindo

Balozi Raphael Haji Lukindo

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kufuatia taarifa za kifo cha Balozi Raphael Haji Lukindo kilichotokea Machi 27, 2012 katika Hospitali ya Saisee iliyopo Mumbai nchini India alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Enzi za uhai wake, Balozi Lukindo alikuwa Mtumishi wa Umma aliyelitumikia Taifa letu katika nyadhifa mbalimbali kuanzia wadhifa wa Shauri yaani District Officer, na kwa muda mrefu amekuwa katika Balozi mbalimbali akiiwakilisha nchi yetu ambapo mara ya mwisho alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan kuanzia mwaka 1983 hadi 1988.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha Balozi Raphael Haji Lukindo ambaye kwa hakika alikuwa Mtumishi wa Umma muadilifu na mchapakazi hodari tangu alipokuwa Bwana Shauri kati ya mwaka 1961 hadi 1962, alipokuwa Afisa katika Balozi zetu za Uingereza na Ujerumani, na hata alipoteuliwa kuwa Balozi akiiwakilisha nchi yetu katika nchi za uliokuwa Muungano wa nchi za Kisovieti za Urusi (USSR), Uingereza, Italia na hatimaye Balozi wa Tanzania nchini Japan kabla ya kustaafu,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete amesema kutokana na utumishi wake uliotukuka, Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye, pamoja na kwamba alikuwa amekwisha kustaafu, lakini ushauri wake ulikuwa bado unahitajika sana hasa katika masuala ya kidiplomasia. Kutokana na msiba huo, Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa familia ya Marehemu Balozi Lukindo kwa kupoteza kiongozi muhimu wa familia.

Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ailaze mahala pema peponi roho ya Marehemu Balozi Lukindo na awape moyo wa uvumilivu na ujasiri wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu katika kipindi chote cha maombolezo. Aidha Rais Kikwete amewahakikishia kuwa yupo pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.