Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal amekutana na mabalozi wapya wa nchi za Saudia, Uturuki na Vatican ambao wamefika ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam leo kujitambulisha na pia kuelezea mipango yao ya utendaji katika kipindi watakapokuwa hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mwandishi wa Makamu wa Rais, Bonifasi Makene, alisema Dk. Bilal alianza kuonana na balozi mpya wa Saudia, Hani Abdullah Mo’minah, ambaye amezungumzia juu ya harakati za Saudia kuhakikisha inakuza uhusiano wa kibishara na Tanzania.
Alisema katika hili ameelezea mkakati wake wa kwanza kuwa ni kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka Saudia ili waungane na wenzao wa Tanzania katika kubadilishana ujuzi na kutanua nafasi zao za kuwekeza katika nchi hizi mbili.
Pia Balozi Mo’minah alizungumzia juhudi za ubalozi wake katika kuwa na makazi ya kudumu, jambo ambalo amelielezea kuwa litawapunguzia gharama za uendeshaji ofisi yao hapa Dar es Salaam. Katika suala jingine, Balozi Mo’minah alisisitiza kuhusu uhusiano katika michezo na akaelezea kufurahishwa kwake na uwanja wa kisasa wa Taifa ambao ameuelezea kuwa unaweza kuhamasisha utalii katika sekta ya michezo hivyo kuliongezea taifa tija.
Kwa upande wake Dk. Bilal alimueleza Balozi Mo’monah kuwa, Tanzania ina uhusiano mzuri na Saudia na lengo la nchi yetu ni kudumisha uhusiano huo, hivyo atafurahi kuona wafanyabiashara wa nchi hizi mbili wanakutana na kubadilishana uzoefu ili kukuza sekta hiyo kwa faida ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake Balozi wa Uturuki nchini, Balozi Ali Davutoglu yeye alimueleza Makamu wa Rais kuwa, Uturuki ipo tayari kuwekeza katika ujenzi wa Chuo Kikuu ili kukuza sekta ya elimu nchini hali inayotokana na shule kadhaa zinazomilikiwa na Waturuki zilizo katika viwango vya shule za Awali, Msingi na Sekondari kuonekana kufanya vema katika mitihani ya kitaifa.
Pia alisisitiza kuhusu kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki ambalo linatarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu, na akasema kongamano hili lina lengo la kuonesha fursa zilizopo katika nchi hizi mbili ambazo zimekuwa zikibadilishana bidhaa za kiuchumi kwa kiwango cha juu. Uturuki ni maarufu katika sekta ya Ujenzi lakini pia inawekeza nchini katika uchimbaji wa Shaba wilayani Mpanda katika mkoa wa Katavi.
Makamu wa Rais alimuelezea Balozi Davutoglu kuwa, uwekezaji katika elimu sasa utazame katika kuzalisha wataalamu hasa walimu wa kuweza kufundisha vyuo vyetu vya Elimu ya juu na kwamba anaamini Uturuki inao uwezo wa kufunza wataalamu hao hasa katika maeneo ya Sayansi.
Balozi wa mwisho kumtembelea Makamu wa Rais alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini, Fransisco Montecillo Padilla, ambaye ameisifia Tanzania katika eneo la kutunza amani na akasisitiza kuwa Vatican siku zote inahamasisha kuhusu usawa na haki pamoja na kuihamasisha jamii kubakia katika amani kwa kuwa huo ndio msingi wa maendeleo.
“Tunafanana katika malengo, tunafanana katika mipango na tunafanya kazi moja ya kuhakikisha kuwa tunajenga jamii yenye kuheshimiana, kuthaminiana na kupendana na inayofanya kazi kwa kujibidisha ili kupata maendeleo,” alisema Dk. Bilal.
Sambamba na hilo, Makamu wa Rais alimshukuru Balozi wa Vatican nchini hasa katika mchango wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma za maendeleo na akamsisitiza kuhusu kutosita kufanya kazi hizo kwa kuwa wananchi wa Tanzania wanazithamini sana na wanatambua mchango huo.