Na Aron Msigwa, MAELEZO
UONGOZI wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es Salaam umesema utaanza kuchukua hatua kwa mwanafunzi au mfanyakazi yeyote atakaye kuja chuoni hapo na mavazi yasiyo ya heshima, huku ukitoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo ili kujenga taifa lenye maadili.
Akizugumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Chuo cha CBE, Athman Ally Ahmed amesema chuo kimefikia uamuzi huo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya uvaaji wa mavazi yasiyo na staha vinavyofanywa na wanafunzi wa kike na wa kiume wawapo chuoni.
Amesema wanafunzi ambao wengi wao ni vijana chuoni hapo wamekuwa mstari wa mbele katika kuiga kila aina ya vazi kutoka tamaduni za watu wa magharibi hali ambayo ameielezea kuwa ni ukiukaji wa mila, desturi na tamaduni za mtanzania.
“Mtindo huu wa kuiga tamaduni za magharibi pasipokuangalia wapi tuna kwenda haukubaliki hata kidogo, ukiangalia katika vyuo vingi vya elimu hapa nchini wanafunzi wamekuwa wakivaa mavazi ya ajabu na yasiyofaa kabisa katika maeneo ya chuo,” amesema.
Amesema kuwa Chuo hicho kimekaa na kubuni sera ili kuyaondoa mavazi ambayo hayaruhusiwi kuvaliwa katika maeneo ya chuo na kubuni sera ya mavazi kwa ajili ya wanafunzi hali itakayowajengea nidhamu wasomi hao wa fani mbalimbali pindi watakapomaliza masomo yao chuoni hapo.
Amefafanua kuwa adhabu mbalimbali zitatolewa kwa wanafunzi watakaokiuka agizo la uvaaji wa mavazi yenye heshima amabazo ni pamoja na kuzuiwa kuingia getini kwa mwanafunzi husika kuingia katika eneo la chuo kwa wale wanaotoka nje ya hosteli na wale wanaoishi ndani ya eneo la chuo hawatapewa huduma yoyote kama vile kuingia darasani, kantini, maktaba au ofisi yoyote ya chuo.
Aidha amefafanua kuwa wanafunzi ambao hawatakua tayari kufuata utaratibu huo watafikishwa mbele ya kamati ya nidhamu huku akibainisha kuwa adhabu itakayotolewa ni mwanafunzi kusimamishwa chuo kwa muda wa miezi mitatu.
Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo hicho ambaye pia ni mkurugenzi wa mafunzo Bi. Bertha Kipillimba amesisitiza kuwa zoezi hilo litawahusu wafanyakazi wote wa kampasi ya Dar es salaam na wanafunzi zaidi ya 6000 wa chuo hicho.
Amesema hivi sasa taratibu hizo za uvaaji wa mavazi yenye staha zimeingizwa kwenye kanuni za chuo na kuongezwa kwenye masharti ya fomu za kujiunga na chuo hicho huku akifafanua kuwa tayari wametoa kipindi cha wiki mbili kwa utekelezwaji wa kanuni hizo na watakaokiuka kuadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Naye mlezi wa wanafunzi wa hicho (Dean of Students) Bw. Faustin China amefafanua kuwa umefika wakati wa wanafunzi hao kujitambua huku akisisitiza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakinyoshewa vidole na jamii kuhusu suala la uvaaji na mienendo ya wanafunzi chuoni hapo.
“Tumesemwa vibaya kwa muda mrefu hatuwezi kuachia suala hili likaendelea, tunataka wanafunzi wetu wavae vizuri kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea ili kujenga heshima ya chuo” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na uanzishawaji wa sera ya mavazi chuoni hapo wakieleza kuwa inaingilia uhuru wao wa kuamua huku wengine wakiupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuliona suala hilo na kulichukulia hatua ili kuleta na kulinda heshima ya chuo hicho.