Na Joachim Mushi, Kisarawe
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) leo umepeleka baadhi ya waandishi wa habari za uchunguzi wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani kuangalia matokeo ya utafiti walioufanya mwaka 2010 juu ya baadhi ya huduma za jamii hasa za afya na maji eneo hilo.
Akizungumza wilayani Kisarawe Ofisa Habari wa TGNP, Kenny Ngomuo alisema wameamua kupeleka baadhi ya waandishi wa habari kuangalia mrejesho wa utafiti walioufanya mwanzoni mwa mwaka 2010 kuangalia huduma mbalimbali za msingi kwa jamii.
Mwaka 2010 TGNP ilipeleka timu ya waandishi wa habari wilayani Kisarawe kufanya uchunguzi na kuibua kero mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili wakazi wa eneo hilo.
Akitoa taarifa fupi kwa wanahabari na waandishi wa habari na wanaharakati Bi. Ngomuo alisema waandishi hao watatembelea vijiji mbalimbali ambavyo vilihusishwa katika uchunguzi wa awali na kuangalia tofauti iliyopo sasa ikiwa ni miaka takriban mitatu tangu kufanyika kwa uchunguzi wa awali.
Alisema waandishi hao watafanya mahojiano na wananchi, wanaharakati na baadhi ya viongozi wa kata zilizofanyiwa utafiti kuangalia tofauti iliyopo tangu kufanyika kwa uchunguzi wa awali, ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo ya huduma za jamii katika maeneo hayo.