Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, jana amefanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kueleza ipo ishara njema ya mabadiliko endapo tabia ya kufanya kazi kwa mazoea itakoma ‘Business as Usual’.
Dk. Shein aliyasema hayo jana huko ukumbi wa Salama, Bwawani, katika Mkutano wa Majumuisho ya Ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Mjini Magharibi kati ya tarehe 21 na 22 mwezi huu ambapo ziara kama hiyo aliifanya hapo Mei mwaka jana.
Dk. Shein alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliopatikana bado kuna mambo ambayo inapaswa kuyachukulia hatua ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira na uzuiaji wa wanyama wanaozurura. Alikiri kuwa kuna mafanikio katika mambo hayo lakini bado jitihada zaidi zinahitajika na kueleza kuwa anafahamu ya kuwa Baraza la Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi wana mikakati yao lakini hiyo haiwezi kufanikiwa kama hawataungwa mkono na wananchi wote pamoja na taasisi.
Alisema kuwa Serikali imeamua kuiendeleza sekta ya Utalii kwani imebaini kuwa sekta hiyo inasaidia sana katika kukuza uchumi nchini lakini inasikitisha kuona moja kati ya malalamiko makubwa ya wageni wanaoitembelea Zanzibar ni suala la uchafu wa mji.
“Baraza la Manispaa litoe leseni za biashara kwa mujibu wa sheria za biashara na kwa wafanya biashara tuache kuweka bidhaa zetu chini hasa katika kipindi hichi cha mvua, uchafu sio tu chanzo cha maradhi mengi bali huondoa haiba ya mji’,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali haiwachukii wafugaji na haina lengo la kuwa na mgogoro nao lakini ina jukumu la kusimamia sheria na ni vyema kwa wenye wanyama wanaozurura ovyo wakawa raia wema na kuacha tabia ya kutumia nguvu wanyama wao wanapochukuliwa.
Dk. Shein alikemea tabia ya wananchi wanaojenga mabondeni na kueleza kuwa wanapokatazwa kujenga katika maeneo kama hayo wajue kuwa sio kwa lengo baya ila ni kuyanusuru maisha na mali zao na kuutaka uongozi wa Mkoa na Wilaya kutoa elimu kwa wananchi juu ya kadhia hiyo na wasibakie maofisini tu.
Pia, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa ya Mkoa juu ya hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa huo imezidi kuimarika na kueleza kuwa hali hiyo inatokana na juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na ushiriki wa wananchi katika shughuli za ulinzi na kusisitiza haja ya kuendeleza utaratibu wa ulinzi shirikishi katika jamii.
Dk. Shein pia alisema kuwa juhudi za serikali ya kuimarisha miundombinu ya barabara isiwe ndio tatizo la kuzidisha ajali hapa na kuwataka wenye vyombo kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Kwa upande wa elimu Dk. Shein alipongeza juhudi za wananchi wa Kianga na kueleza kuwa ziara yake hiyo ambayo aliweka jiwe la msingi katika madarasa matano ya skuli ya Kianga ilimpelekea kujua kuwa bado kuna taasisi zinafanya kazi kwa mazoea likiwemo Shirika la umeme la Zanzibar (ZECO) kwa kuchelewa kupelekea huduma hiyo katika skuli hiyo hadi majuzi alipofanya tena ziara yake ikiwa ni zaid ya miaka saba.
Kwa upande wa sekta ya maji Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji na kueleza kuwa hadi mwaka 2013 tatizo la maji litapungua ama kuondoka kabisa na kuipongeza ZAWA huku akisisitiza haja kwa Mamlaka hiyo kutoa elimu juu ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa viongozi na wananchi wa Jimbo la Jangombe kwa uwamuzi wao wa kimaendeleo wa kutaka kuwasogezea wananchi huduma ya afya kwa kkukifufua kituo cha afya cha ‘Jumba la vigae’ ambacho kina historia kubwa kiafya.
Sambamba na hayo, Dk Shein alirejea kauli yake aliyoitoa katika ziara yake ya mwaka jana kwa kuwataka viongozi wa Mkoa, Wilaya na Wizara kuitatua migogoro ya ardhi iliomo katika maeneo yao kwani imesababishwa na wao wenyewe.
Alisema kuwa mwaka jana alipokuwa katika ziara kama hiyo wakati akifanya majumuisho yake mnano mwezi Mei katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Tunguu alilielezea suala hilo na kuwaeleza viongozi hao lakini amegundua bado tatizo hilo lipo.
Kwa upande wa kuwatunza na kuwaenzi wazee, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea nalengo la Mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo mwasisi wake marehemu Mzee Karume aliamua kujenga makaa maalum kwa ajili ya wazee.
Dk. Shein alieleza kuridhika na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto katika kuimarisha huduma za wazee na kuahidi kuwa ataziimarisha huduma hizo kwa kuwapelekea Daktari, gari, huma za maji, kuhakikisha wanakula mlo wa kutwa kwa taratibu nzuri na kufanywa ukarabati mkubwa wa ukumbi na jiko lao sanjari na ulinzi wa uhakika ambao tayari upo.