Na Joachim Mushi
WAZIRI wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Tanzania, Samuel Sitta ametoboa siri kuwa anania ya kugombea nafasi ya urais mwaka 2015, na kuwashangaa watu wanaomuofia yeye kugombea nafasi hiyo.
Amesema ni haki ya kila Mtanzania mwenyesifa kugombea nafasi hiyo, hivyo kuwataka baadhi ya watua waache kuwanyooshea vidole wengine na kutoa sababu zisizokuwa za msingi.
Sitta ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza kwenye tamasha la waandishi wa habari (Media Day), lililofanyika Ukumbi wa Msasani Beach jijini Dar es Salaam.
“…La mwisho na hili ni la jumla, watu huwa wanapata kiwewe wakisikia Samuel Sitta anataka kugombea urais, mimi siwaelewi maana ni haki ya kila Mtanzania kugombea urais…na mara nyingine wana mnukuu Rais (Rais Jakaya Kikwete) eti anataka apate rais (ajaye) kijana, mimi sio kijana (Sitta)…lakini Watanzania ndiyo watakaoamua ni nani anafaa wakati utakapofika ,” alisema Sitta.
Kwa kauli hiyo inaonesha wazi kuwa Waziri Sitta huenda akaingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais mwaka 2015, kama baadhi ya wachambuzi wa mambo wanavyotabiri.
Aidha alisema mwaka 2015 Tanzania inaitaji kiongozi mwenye muelekeo mpya na si kuwa na viongozi ambao ni wababaishaji, wala rushwa na wabadhirifu wa fedha za umma hali ambayo imeifanya rushwa kuonekana jambo la kawaida kwa jamii na kuendelea kuliathiri taifa.
Amesema rushwa imetawala katika miradi mbalimbali nchini hivyo kuendelea kuligharimu taifa. Ameongeza kuwa rushwa ndio imeifanya Tanzania kushindwa kuwa na umeme wa uhakika hadi sasa huku ikitapeliwa na wawekezaji wajanja kwa maslahi ya wachache.
“Rushwa ni hatari kubwa sana ndugu zangu, ndiyo inayofanya miradi yetu iwe ghali sana, miradi yetu isiwe na ajira ya kutosha wala tija, rushwa inafanya kampuni zinazokuja kuwekeza ziwe za kitapeli…nchi yetu imekuwa na umeme wa tabu bila sababu, sisi (Tanzania) ni nchi ya pili katika Afrika kuwa na rasilimali za kutosha kuweza kuzalisha umeme,” alisema Sitta na kuongeza kuwa endapo vyanzo vya umeme vingetimika ipasavyo Tanzania ingelikuwa ikiuza umeme kwa mataifa mengine ya Afrika.
Hata hivyo katika kauli zake zote Sitta hakumtaja kiongozi wala kundi lolote ambalo linaonesha kiwewe dhidi yake kwa hofu ya kugombea nafasi ya urais mwaka 2015.