Mheshimiwa Mhandisi Gerson H. Lwenge (Mb), Naibu Waziri wa Maji;
Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Iringa;
Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa;
Washirika wetu wa Maendeleo katika Sekta ya Maji; na
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana: Shukrani
Ninakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji kwa kunialika nije kujumuika na ndugu zetu wa Iringa katika sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani. Mwaka huu, maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa hapa mkoani Iringa. Nakushukuruni viongozi na wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hizi. Huu ni wajibu mkubwa na natoa pongezi nyingi kwenu nyote kwani mmeutekeleza vizuri. Maandalizi yamekuwa mazuri, na sherehe zimefana. Wahenga walisema “usione vinaelea vimeundwa”. Ushirikiano mzuri uliokuwepo baina ya viongozi wa Wizara ya Maji na uongozi wa mkoa wa Iringa ndiyo siri ya mafanikio. Tafadhali dumisheni na endelezeni ushirikiano na mshikamano wenu kwa hili na mengine. Ahsanteni sana, na hongereni sana.
Napenda kutoa pongezi maalum kwa wananchi wa Iringa kwa kufika hapa kwa wingi kushiriki katika kilele cha maadhimisho haya kitaifa. Kufika kwenu ndiyo ukamilifu wa shughuli hii na mafanikio yake. Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa michango na misaada yao adhimu. Marafiki zetu wametuunga mkono katika juhudi zetu za kuongeza upatikanaji wa maji na huduma ya usafi wa mazingira mijini na vijijini. Aidha, wamekuwa wanatoa mchango mkubwa katika kuboresha uwezo wetu wa kusimamia rasilimali maji nchini. Ninawaomba, Waheshimiwa Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa waliopo hapa, wazipokee na kuzifikisha shukrani zetu za dhati, kwa wakuu wa nchi zao na mashirika yao.
Umuhimu wa Maadhimisho
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho haya ya Siku ya Maji Duniani, ambayo yanafanyika kila mwaka, sasa yamezoeleka, na ni ushahidi wa umuhimu ambao Serikali na wananchi wanaoutoa kwa sekta ya maji. Kote duniani siku ya leo watu wanakumbushana umuhimu wa matumizi bora na endelevu ya maji kwa ajili ya wanadamu, wanyama, mimea na viumbe hai wengine. Aidha, ni muhimu sana kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Maadhimisho haya pia yanatoa nafasi kwa wadau kujadili mafanikio yaliyopatikana na matatizo yaliyopo katika kuendeleza sekta ya maji na jinsi ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwa pamoja, kama taifa, tunapata fursa ya kufanya tathmini ya tulikotoka, tulipo sasa na kuainisha malengo na mipango yetu kwa siku zijazo.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho
Ndugu Wananchi;
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ina ujumbe mzito sana: “Maji kwa Usalama wa Chakula”. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila ya maji chakula hakuna. Chakula ni matokeo ya kilimo na kilimo hakiwezekani bila ya maji. Maji hayo yanaweza kutokana na mvua ya Mwenyezi Mungu au juhudi za mwanadamu za kuyachukua kutoka chini au juu ya ardhi, katika mito, maziwa na mabwawa na kuyafikisha shambani.
Kwa kutambua ukweli huo kuhusu maji, katika siku ya leo na katika wiki yote hii tafakuri zetu zilielekezwa kwenye kutafuta mikakati na mbinu za kuhakikisha kuwa maji kwa ajili ya kilimo yanapatikana ya kutosha. Naomba tutambue kuwa mkakati wowote kwa ajili hiyo hauna budi ujielekeze katika kufanya mambo yafuatayo: Kwanza kabisa, kuhifadhi mazingira ili mvua ziwe nyingi na vyanzo vya maji viwe salama. Kama sote tunavyoona na kufahamu kuwa siku hizi upatikanaji wa mvua si wa uhakika kama ilivyokuwa zamani. Majira hayatabiriki na mvua si za kuaminika. Miaka ya nyuma tarehe na mwezi wa mvua kuanza na kwisha vilikuwa vinajulikana. Siku hizi hapana. Kilimo kimekuwa shughuli ya mashaka makubwa.
Ndugu Wananchi;
Uharibifu wa mazingira uliotufikisha hapa unatokana na shughuli za wanadamu. Tumekata misitu kupita kiasi ama kwa shughuli za mbao au kilimo. Aidha, katika nchi zilizoendelea shughuli za viwanda vimechangia kuongeza gesi-mkaa katika anga na joto kuongezeka duniani na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi na madhara yote tunayopata sasa.
Kwa hiyo ndugu zangu ni muhimu sana katika siku ya leo kusisitiza hifadhi ya mazingira na kukumbushana kuhusu kutunza misitu na pale ilipoharibiwa tupande miti tena. Tutunze vyanzo vya maji kwani vinatuhakikishia kuwepo kwa rasilimali ya maji kwa miaka mingi ijayo na kwa kiwango cha kutosha. Tusipofanya hivyo mvua itaendelea kupungua na maji pia yatapungua kiasi cha kusababisha chakula na mahitaji mengine kupungua.
Ni ukweli ulio wazi kwamba maji yanapungua kwa kasi. Ninyi wa Iringa ni mashahidi. Nani kati yenu alifikiria mto mkubwa kama Ruaha ungeweza kukauka? Sasa si jambo la kufikirika tena. Tujiulize kwa nini? Tujiulize je, inawezekana ukarudi katika hali yake ya zamani? Kama ndiyo kwa vipi? Tuhifadhi mazingira toka unakoanzia na kote unakopita. Nawataka, Wizara za Maji, Maliasili na Mazingira pamoja na mikoa ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Singida, Rukwa na Ruvuma kulipa kipaumbele suala hili.
Jambo la pili naomba tutumie kwa ufanisi, kiasi kidogo cha maji kilichopo ili kiweze kuzalisha chakula kinachotosheleza mahitaji ya sasa na ya baadaye. Pia yaweze kukidhi mahitaji mengine kwa matumizi ya wanadamu na uchumi. Haya ni mambo yanayowezekana. Utaalamu upo, teknolojia ipo na wataalamu wapo wanaoweza kuelekeza jamii kuyafanya hayo. Lazima tufanye kila tuwezalo kufanikisha jambo hili. Aidha, mikakati ya pamoja ya wadau kuhimiza matumizi ya teknolojia zinazoweza kuzalisha chakula kwa wingi kwa kutumia maji kidogo haina budi kuandaliwa.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto
Ndugu Wananchi;
Naibu Waziri ameeleza jitihada zinazofanywa na Serikali kukabili changamoto zinazopelekea kupungua kwa maji. Sikusudii kuzirudia, hata hivyo nisisitize mambo yafuatayo kuhusu kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kukuza uzalishaji wa chakula nchini:
(i) Kutafuta teknolojia za kilimo zenye tija kubwa ili kuwajengea uwezo wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kutumia maji kidogo. Tayari tumekwishafanya mazungumzo na rafiki zetu wa India watusaidie kwenye eneo hili;
(ii) Kuweka mkakati maalum wa kuendeleza teknolojia bora za uvunaji wa maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya majumbani, matumizi ya taasisi kama shule, vituo vya afya, hospitali na zahanati; na kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa chakula. Hii ni kazi tuliyokwishaianza na tutaendelea nayo;
(iii) Kuyatambua maeneo yatakayoweza kuongeza matumizi ya maji ya visima kwa ajili ya kuboresha kilimo cha umwagiliaji hasa katika maeneo kame. Tayari tumekwishaanza kazi hii kupitia mpango wa usambazaji maji vijini. Tunaendelea nao mpango huu;
(iv) Kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji kwa kuwaelimisha wakulima mbinu za kitaalam za kudhibiti mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mtiririko wa maji hasa wakati wa mvua kubwa ambao husababisha kupungua kwa rutuba. Hii ni kazi ambayo tunaendelea nayo;
(v) Kufanya utafiti wa mbegu za mazao ya chakula zenye uwezo wa kuhimili ukame ili kuhakikisha usalama wa chakula. Tumekwishaanza na tunaendelea na utafiti huo kupitia vituo vyetu vya utafiti nchini.
Ni matumaini yangu kwamba, kwa kuchukua hatua nilizotaja, tutaweza kukabiliana na changamoto za upungufu wa maji ambazo zinatishia ustawi wa wananchi na jamii yetu kwa ujumla.
Jitihada nyingine za Serikali kuboresha Huduma za Maji
Ndugu Wananchi;
Serikali imeendelea na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha huduma ya maji nchini. Kwa upande wa huduma za maji, mipango ya utekelezaji ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira niliyoizindua mwaka 2007, ililenga kuongeza upatikanaji wa huduma za majisafi na salama katika miji mikuu 19 ya mikoa (ukiacha Dar es Salaam na Pwani) kutoka asilimia 78 mwaka 2006 hadi asilimia 90 mwezi Desemba mwaka 2010. Hadi ilipofika Desemba 2011, hali ya upatikanaji wa huduma za majisafi na salama katika miji hiyo ilikuwa asilimia 88, ikiashiria kuwa licha ya kwamba hatukufikia lengo, lakini hatukuwa mbali, tulikaribia sana kufikia lengo.
Katika maeneo ya vijijini, lengo lilikuwa kuongeza upatikanaji wa huduma za maji kutoka asilimia 55 mwezi Desemba mwaka 2006 hadi asilimia 65 ifikapo mwezi Desemba 2010. Baadaye kutokana na mapitio yaliyofanyika ya Programu ya mwaka 2010/2011, lengo hili limerekebishwa na kuwa asilimia 62 ifikapo mwezi Desemba 2012. Hadi Desemba 2011, upatikanaji wa huduma za maji vijijini ulikuwa katika wastani wa asilimia 58, ikiashiria kuhitajika kwa juhudi za ziada ili tuweze kufikia lengo. Juhudi hizo za ziada ni pamoja na zile zinazohitajika kutekelezwa ili kuboresha huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam, katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo.
Ndugu Wananchi;
Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo inaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kutekeleza miradi ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini. Serikali imeshakamilisha ujenzi wa miradi ya maji kwa miji ya Mbeya, Mwanza na Kibiti. Miradi ya miji ya Kigoma, Lindi, Musoma, Bukoba, Dodoma na Sumbawanga fedha zake zimeshapatikana. Sasa hivi Makandarasi wanatafutwa kwa ajili ya ujenzi. Aidha, mradi wa majisafi kwa mji wa Orkesmet ujenzi wake utaanza mwezi Julai, 2012.
Mradi wa maji wa Pawaga niliouzindua jana na Mradi wa Majisafi na taka niliouzindua leo asubuhi hapa Iringa ni mwendelezo wa juhudi hizo za Serikali. Mradi wa maji wa Pawaga ulianza kutekelezwa mwezi Aprili mwaka 2008. Mradi huo upo umekamilika ingawaje bado zipo kazi za kufanya hasa kuhusu chujio, nyumba ya mhudumu na nyumba ya kuhifadhia madawa ya kusafishia na kutibu maji. Aidha, kuna kazi ya ujenzi wa matangi matatu ya vijiji vya Magozi, Mkombilenga na Mboliboli na ukarabati wa matangi mawili ya Luganga na Itunundu.
Jana tulipokuwa Pawaga, nilitoa shukrani zangu na za Serikali kwa ndugu zetu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Iringa kwa kubuni na kutekeleza mradi huu unaowapatia maji ya uhakika wananchi 22,500 wa Kata za Itunduru na Kilolompya. Nilieleza kuwa ni kielelezo kingine cha mchango muhimu unaotolewa na Kanisa hilo mkoani na kwingineno nchini. Nimemhakikishia Baba Askofu Mugomi kuwa Serikali kwa upande wake itaongeza mchango wake katika hatua zifuatazo za kukamilisha na kuendeleza mradi huu. Pia tutaendelea kushirikiana na Kanisa la Anglikana katika shughuli nyingine wazifanyazo mkoani na nchini.
Ndugu Wananchi;
Mradi mwingine ni ule niliouzindua leo wa kuboresha huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka mjini Iringa. Mradi huo nao ulianza kutekelezwa mwezi Agosti 2008 na ulikamilika mwezi Novemba 2011. Mradi umetekelezwa kwa gharama ya Euro 33,188,000 sawa na shilingi bilioni 73. Kati ya fedha hizo, Jumuiya ya Ulaya (EU) ilichangia Euro 17,076,000 (Shilingi Bilioni 37.6); Serikali ya Ujerumani ilichangia Euro 446,000 (Shilingi Milioni 982); na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ilichangia Euro 15,666,000 (Shilingi Bilioni 34.5).
Mradi huu unaweza kutosheleza mahitaji ya maji kwa wakazi 300,000. Hivi sasa mji wa Iringa una wakazi 173,000. Mradi huu una uwezo wa kutosheleza mara mbili ya watu waliopo sasa. Kwa miaka mingi ijayo maji si jambo la wasiwasi Iringa. Kabla ya mradi huu hali ya upatikanaji wa majisafi na salama ilikuwa si ya kuridhisha. Mradi huu pia, utaunganisha wakazi 4,200 zaidi kwenye mfumo wa majitaka. Miongoni mwa manufaa ya mradi huu ni kuongeza hali ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Iringa kutoka asilimia 68 mwaka 2007 hadi asilimia 95 kwa sasa. Mradi pia, umeboresha mindombinu ya uondoaji wa majitaka kutoka asilimia 12 mwaka 2007 hadi asilimia 14 za sasa.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kwamba mafanikio haya yatakuwa ni kichocheo cha kumfanya kila mwana-Iringa aweze kuunganishwa kwenye huduma za majisafi na salama. Pia, itakuwa rahisi kuunganishwa kwenye huduma za uondoaji wa majitaka kwa walio karibu na mtandao wa majitaka kwa watu kutumia utaratibu uliowekwa na Mamlaka husika. Nawaomba wananchi shirikianeni na Mamlaka za Serikali kuhakikisha kuwa miundombinu ambayo imejengwa kwa gharama kubwa inalindwa muda wote ili isiharibiwe na watu wenye nia mbaya.
Ndugu zangu, nawaomba wana-Iringa Mjini pamoja na wakazi wa mijini kwa ujumla kote nchini kulipia ankara za maji mara zinapofikishwa. Fedha hizo zinahitajika kuhakikisha kuwa huduma za majisafi na uondoaji majitaka zinakuwa endelevu.
Ushirikishwaji wa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Vilevile, ni muhimu ndugu wananchi mkaelewa kwamba wakati Serikali inatimiza jukumu lake la kuhakikisha kila mmoja wetu anapata maji, na nyinyi pia mnao wajibu wa kuhakikisha kwamba maji yanatumika ipasavyo na ikibidi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Aidha tunapaswa pia kuongeza ushirikishwaji wa wadau katika maamuzi, lakini yawe maamuzi yanayozingatia matokeo yake kwa siku zijazo. Maana, wataalam wanatutahadharisha kuwa inawezekana katika karne ya 21 maji yakawa na thamani au hata kusababisha magomvi, kama ilivyokuwa kwa mafuta katika karne ya 20. Ushirikishwaji ni jambo jema. Tumekwishalianza sehemu mbalimbali nchini na ni muhimu tuendelee nalo.
Mwisho
Ndugu Wananchi;
Nimesema mengi. Naomba nimalizie kwa kuwatakia maadhimisho mema na natarajia kuwa uzoefu na mafanikio katika maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa mkoani Iringa yatatoa changamoto kwa wengine na yataigwa na mikoa mingine.
Baada ya kusema hayo, ninapenda kutamka kuwa Maadhimisho na Maonesho ya 24 ya Wiki ya Maji Kitaifa mwaka 2012 yamehitimishwa rasmi hapa mjini Iringa.
“ASANTENI KWA KUNISIKILIZA”