KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom leo imemkabidhi askari polisi, Peter James Kilalo hundi ya kitita cha sh. milioni 10 kama mshindi wa droo ya mwezi ya promosheni ya M-PESA inayoendeshwa na kampuni hiyo.
Kilalo amekabidhiwa hundi hiyo leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza katika hafla fupi iliyohudhuriwa pia na waandishi wa habari.
Akipokea hundi yake Kilalo ambaye ni Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kituo Kikuu cha Dar es salaam, ameshukuru kwa kuibuka mshindi jambo ambalo amesema hakulitegemea.
“Kwa kweli mimi ni mteja mzuri wa M-PESA lakini sikutegemea kwamba ningeibuka mshindi, ila sasa ninapopokea hundi hii naamini kwamba nimeshinda na fedha hizi milioni 10 ni zangu,” alisema Kilalo.
Alipoulizwa namna alivyojipanga kutumia pesa hizo, Kialalo alijibu; “Jamani mimi ni masikini na sikuwahi kuota kwamba ipo siku nitashinda kiasi kikubwa cha fedha namna hii hivyo jambo kubwa kwangu kwa wakati huu ni kwanza kuacha akili yangu itulie kabisa ndio niamue niziwekeze wapi ili zinikwamue kimaisha,” alisema.
“Nina mawazo kadhaa ya biashara ambayo nimekuwa nikiyawaza kama njia ya kutafuta namna ya kujikwamua kimaisha hivyo hizi pesa nitazielekeza huko ila baada ya akili yangu kwanza kutulia kutoka katika hali ya furaha niliyonayo sasa.” Aliongeza
Mshindi huyo ametumia pia fursa hiyo kuwashauri watanzania kutumia huduma ya M-PESA kwa kuwa mbali na kwamba imerahisisha maisha katika utumaji na upokeaji fedha mijini na vijijini bado wanaweza kuwa katika nafasi ya kushinda kama yeye
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza amesema promosheni hiyo imelenga kuwawezesha wateja wa M-PESA kubadili masiha kutokana na wanavyotumia huduma hiyo.
“Promosheni hii tulizindua mwezi uliopita tukilenga kuwawezesha wateja wetu kujishindia zawadi za fedha taslimu, kiasi cha sh. milioni 480 kinashindaniwa ambapo hadi sasa wateja zaidi ya 4,000 wameshajinyakulia zaidi ya sh. milioni 120,” alisema Rene.
AmesemaVodacom inatambua umuhimu wa huduma ya M-PESA katika maisha ya kila siku ya wananchi na hivyo wakati wote imekuwepo mikakati imara ya kuiwezesha huduma hiyo kuendelea kuwa bora zaidi,salama na ya kuaminika sokoni.
“Matumizi ya huduma ya M-PESA hapa nchini yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana, kiwango cha wananchi kutuma na kupokea pesa pamoja na kufanya malipo ya bidhaa mbalimbali kupitia M-PESA ni kikubwa jambo ambalo linakuwa rahisi zaidi kutokana na mtandao mpana tulionao wa mawakala wanaofikia 20,000 mijini na vijijini.” Aliongeza Bw Rene
Promosheni hiyo itadumu kwa siku tisini kutoka Februari 13, 2012 hadi Mai 13, 2012. Mbali na kutoa mshindi mmoja wa shilingi milioni kumi kila mwezi pia kila siku washindi mia moja hujishindia Sh. 50,000 kila mmoja.