TAMWA kufanya Mkutano Mkuu Jumamosi

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya akisisitiza jambo kwenye moja ya mikutano ya chama hicho.

MKUTANO Mkuu ambao ndicho chombo cha juu kinachotoa maamuzi kuhusu sera na mipango ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania–TAMWA, unatarajiwa kufanyika Machi 24, 2012 katika ofisi zake zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

Kwa mujubu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema Wanachama wanawake wapatao 100 watashiriki katika mchakato wa kujadili na kuafiki mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya chama, ambapo maazimio yake yatapelekwa kwenye Mkutano Mkuu Machi 24 mwaka huu kwa maamuzi.

Nkya alisema katika Mkutano Mkuu wanachama hushiriki katika maamuzi mbalimbali ya chama ikiwemo kupitisha ripoti ya kazi, mahesabu pamoja na kuchagua viongozi wa ngazi anuai kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kichama.

Wanahabari hao mwaka huu watapata fursa ya kumchagua Mwenyekiti wao mpya ambaye ndiye msimamizi wa Mkutano Mkuu na mikutano yote ya Bodi ya TAMWA kutokana na aliyekuwepo kumaliza muda wake. TAMWA ambayo ilianzishwa na wanahabari wanawake 12 miaka 25 iliyopita, sasa ina wanachama wanawake wapatao 100 wanaofanya kazi kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

“Tangu chama kilipoanzishwa kimekuwa kikipokea na kuhudumia watu wengi hasa wanawake na watoto ambao wamekumbwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiwemo wanawake kudhulumiwa mirathi, ubakaji, ukeketaji, wanawake kutelekezwa na ndoa za utotoni,” alisema Nkya katika taarifa hiyo.

Aidha chama kimekuwa kikijishughulisha na shughuli mbali mbali kupitia vyombo vya habari vya magazeti na Television katika kuharakisha maendeleo ya wanawake, watoto hasa wa kike na taifa kwa ujumla.