Moshi
WANACHAMA wa Vyama vya Ushirika mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuwawajibisha viongozi ambao si waadilifu ikiwa ni pamoja na kuwaondoa madarakani hatua ambayo itasaidia kuondoa migogoro ya mara kwa mara na kuimarisha vyama vya ushirika.
Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Mrajisi mkoani Kilimanjaro, Kasia Kasia, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake kuhusiana na hali ya ushirika mkoani humo, ambapo alisema kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na migogoro ya mara kwa mara inayochangiwa na viongozi kutokuwa waadilifu.
Kasia alisema viongozi wasio waadilifu na waaminifu katika vyama vya ushirika wanapaswa kuondolewa bila kuonewa huruma na kutafutwa viongozi wengine ambao wataweza kuvijenga vyama na kuviimarisha.
Mbali na hilo aliwataka pia wanachama wa vyama vya ushirika kuepuka kuhongwa na kutumiwa vibaya na viongozi wasio waadilifu ili kuendelea kushikilia nafasi za uongozi jambo ambalo husababisha vyama vya ushirika kushindwa kuendelea mbele.
“Wanachama wa vyama vya ushirika wasisubiri Serikali ijekutatua migogoro iliyoko katika vyama vyao ili hali wao wenyewe wanajua chanzo chake, kama chanzo ni viongozi, wao ndio waliowachagua wanapaswa kuchukua hatua kwa kufuata taratibu ili kuimarisha ushirika na si kukaa kimya na kuilaumu serikali,” alisema Kasia.
Aidha alisema viongozi wazembe na wasio waadilifu hawapaswi kufumbiwa macho bali wanapaswa kuondolewa mara moja na kuchaguliwa viongozi wengine ambao wataweza kuimarisha vyama na kuinua ushirika nchini.
“Uimara wa vyama vya ushirika ni pamoja na kuwa na viongozi waliowaadilifu na waaminifu, waliokubali kujitoa kutumikia ushirika na si wachakachuaji ambao hupenda uongozi kwa maslahi binafsi na si kujenga chama,” alisema Kasia.
Katika hatua nyingine Kasia aliwataka wataalamu wa ushirika mkoani humo kuhakikisha bodi za ushirika zinaimarika na viongozi wa vyama hivyo wanakuwa waadilifu. Alisema vyama vingi vya ushirika katika mkoa huo vimekuwa vikishindwa kusonga mbele kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo kutokuwepo na uaminifu na uadilifu hivyo wataalamu wa ushirika wanapaswa kufuatilia suala hilo na kuhakikisha vyama vya ushirika vinaimarika.
Alisema pamoja na kutokuwepo kwa uadilifu kwa baadhi ya viongozi katika vyama vya ushirika pia vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto ya misukosuko ya kisiasa pamoja na uwezo wa kiuchumi kutokuwa imara.
“Toka kuanza kwa vyama vya ushirika mkoani Kilimanjaro mwaka 1932 ambapo mwaka huu mkoa huu unatimiza miaka 80 ya ushirika, bado tunachangamoto nyingi lakini tunaendelea kupambana nazo ili kuhakikisha zinatatulika na ushirika unakua imara katika mkoa huu,” alisema Kasia.
Migogoro katika vyama vya ushirika mkoani Kilimanjaro ni moja ya sababu ambayo imekuwa ikisababisha vyama vingi kushindwa kuendelea na kufa hali ambayo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na kutokuwepo kwa uadilifu na uaminifu kwa viongozi na hivyo wanachama kushindwa kujiamini na kuwang’oa madarakani licha ya kuwa wao ndio wamewachagua.