Prof. Maji Marefu atishia kulishtaki gazeti Mwananchi

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani a.k.a Prof. Maji Marefu akionesha gazeti la Mwananchi analolilalamikia.

MBUNGE wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani kwa jina maarufu kama Prof. Maji Marefu ametishia kulishtaki gazeti la Mwananchi kwa kile anachodai limechapisha picha yake ndivyo sivyo. Maji Marefu ambaye juzi alidai Mgombe wa Chadema, Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alikuwa amewaamuru wafuasi wa chama hicho kumchoma moto- amesema lalamika kuwa gazeti la Mwananchi limechezea picha yake kwa kumuunganisha na Nassari kwenye picha moja jambo halikuwepo kwenye tukio.

Picha yenyewe anayolalamikia Profesa Majimarefu ndiyo hii kama ilivyonakiliwa kutoka gazeti la mwananchi.

“Picha hii nilipigwa nikiwa na huyu mbunge mwenzangu, Vicent Nyerere (kulia), lakini huyu wa kushoto (Joshua Nassari) hakuwepo karibu yangu kabisa! Yeye alikuwa mbali akiamrisha vijana wanichome moto tena akiwa na hasira, tofauti na anavyocheka katika picha hii. Huu ni mchezo mchafu wa kuunganisha picha kwenye kompyuta uliofanywa na CHADEMA na kwa makusudi gazeti hili likaichapisha, baada ya kuona kwamba hatua aliyofanya Nassari ya kutaka niuawe jana ni mbaya sana. Nitalishitaki gazeti hili,” alisema mbunge huyo leo.

Mbunge huyo wa Korogwe Vijijini, Ngonyani alilalamika wakati akionesha picha inayomuonesha akiwa katika furaha ya hali ya juu yeye, Nyerere na Nassari. Picha hiyo imechapishwa jana ukurasa wa kwanza gazeti la Mwananchi.