Mume amchinja mkewe kama ‘kuku’

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Said Mwema

Na Said Mwishehe
Dodoma

MWANAUME aliyefahamika kwa jina la Lucas Makomela (55) amefanya mauji ya kutisha baada ya kumchinja mkewe, Josephina Tatu (42) kisha naye kuamua kujinyonga.

Akizungumzia tukio hilo jana, mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zolothe Stephen alisema tukio hilo la mauji limetokea usiku wa kumkia jana katika kijiji cha Nala. Alisema Makomela ambaye ni mkulima kijijini hapo aliamua kuumua mkewe na baada ya tukio hilo naye alijitoa uhai kwa kujinyonga.

Kamanda Stephen alisema uchunguzi wa tukio hilo la kutisha unaendelea, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo la mauji.

“Kwa sasa tunaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo na hadi sasa hatujamkamata mtu yoyote kwa mauji hayo kwani aliyehusika na tukio hilo la kuua naye aliamua kujinyonga,” alisema.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma hasa wa eneo la Kijiji cha Nala wamesikitishwa na tukio hilo ambalo wameliita ni la kinyama na lenye kujaa ukatili, kutokana na aina ya mauji aliyofanyiwa mwanamke aliyechinjwa.

Hata hivyo Kamanda Stephen alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu hao kabla ya tukio hilo inawezekana kuna jambo walikuwa hawajakubaliana walipokuwa chumbani na kwamba miili yao ilikuwa haina nguo hali inayoonesha hakukua na maelewa mazuri baina yao.