Dk. Mwakyembe arejea ofisini, asema ugonjwa unachunguzwa

Waziri wa Wizara ya Ujenzi nchini Tanzania, Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam baada ya kuripoti ofisini na kuanza kazi baada ya kurejea kutoka India kwa matibabu

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Wizara ya Ujenzi nchini Tanzania, ameanza kazi leo baada ya kutoka kwenye matibabu ya ugonjwa unaomsumbua kwa muda. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema anamshukuru Mungu amerejea salama hivyo kuomba suala la ugonjwa wake sasa liachwe kuandikwa kwani yu salama.

“Waandishi muache sasa iwe imefika mwisho kuandika kutokana kurudi na kuendelea na majukumu ya kikazi kwanza nina mafaili yananisubili ofisini kwa ajili ya kusaini,” alisema Mwakywembe.

Amesema anamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa karibu naye tangu alipoanza kuugua, pamoja na Serikali yake kwa jitihada walizozionesha katika kipindi chake cha ugonjwa.

Aidha Dk. Mwakyembe amewaondoa wasiwasi Watanzania hasa wapigakura wa Jimbo lake kwamba yu salama na kuwataka wasubiri uchunguzi unaofanywa dhidi ya ugonjwa wake. Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha ameunda tume ambayo inafanya juu ya ugonjwa unaomsumbua.

Hata hivyo amewataka wapiga kura wake wa Jimbo la Kyela kuacha wazo la kuandamana kuja Dar es Salaam kwani ratiba yake ya kwenda jimboni ipo wazi hivyo atatumia muda huo kwenda kuzungumza nao itakapowadia. Amesema kwa sasa hata kama Watanzania wataelezwa ugonjwa unaomsumbua hawata uelewa kutokana kuwa suala la kitaalamu zaidi.