Lowassa, Mbowe vitani Arumeru

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa

CHADEMA WAMVUTIA PUMZI, WASEMA HAWABABAIKI, HANA JIPYA

Arumeru

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Freeman Mbowe amesema chama chake kinamgonja kwa hamu Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha. Kauli ya Mbowe inatokana na habari zilizoenea Arumeru ambazo pia zimethibitishwa na watu walio karibu na Lowassa, zikisema Mbunge huyo wa Monduli (CCM) wakati wowote atatua Arumeru Mashariki kumpigia kampeni mgombea wa chama chake, Sioi Sumari.

“Mzee (Lowassa) ni kweli kwamba ana mpango wa kuja hapa kumpigia kampeni mgombea wetu wa CCM, inaweza kuwa ni wiki ijayo au wiki ile nyingine, nadhani bado anajipanga. Ila taarifa za uhakika ni kwamba atakuja,”alisema mmoja wa makada wa CCM jana asubuhi.

Taarifa za kwamba Lowassa atashiriki kwenye kampeni hizo zilianza katikati ya wiki hii siku chache kabla ya kurejea kutoka Ujerumani.

Kwa upande wake, Lowassa akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, zaidi ya kusema kwamba hivi sasa anapumzika baada ya kurejea kutoka nchini Ujerumani alikokwenda kwa ajili ya matibabu ya macho.

“Kwani vipi……kwa kweli kwa sasa siwezi kusema lolote kuhusu hilo, ndiyo kwanza ninapumzika kama unavyojua nimetoka safari, katika hilo tusubiri kwanza,” alisema mbunge huyo ambaye anatajwa kwamba alikuwa akimuuga mkono Sioi kuanzia kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Kwa upande wake Mbowe akizungumzia taarifa za ujio wa Lowassa alisema: “Tunamsubiri sana kwa hamu, kwani yeye ni nani? Lowassa ni kama mtu mwingine yoyote ndani ya CCM, hivyo yoyote atakayeletwa na CCM wala hatumwogopi, tuko tayari kukabiliana naye.”

Aliongeza: “Kwani Mkapa (Benjamin) si alikuja hapa….akamuulize baada ya kuzindua kampeni za chama chake na kusema maneno yake kilichomtokea ni nini? Kwa hiyo bwana na yeye (Lowassa) ni walewale maana hana tofauti na Mkapa maana wote wanatoka CCM, sisi Chadema hatutishiki hata kidogo.”

Lowassa ni miongoni mwa wazaliwa wa mkoani Arusha wanaotajwa kwamba wanakubalika katika siasa za Arumeru, hivyo ujio wake unaweza kuwa chachu kubwa katika kampeni za CCM kinachopigania kuendelea kushika nafasi ya uwakilishi wa jimbo hilo.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa anatarajiwa kutua Arumeru leo kuongeza nguvu katika kampeni za Chadema ambacho kinawania kujenga heshima kwa mgombea wake, Joshua Nassari kutwaa jimbo hilo.

Tayari CCM wameongeza nguvu za kampeni zake kwa kuwaogeza makada kadhaa, wengi wakiwa ni wabunge wa majimbo mbalimbali wanaoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, hivyo kuongeza chachu ya kampeni hizo.

Wassira amvaa Dk Slaa
Dk Slaa anatua Arumeru kipindi ambacho anasubiriwa kujibu tuhuma zilizotolewa na Wassira ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Arusha.

Wassira katika mikutano mbalimbali ya kumnadi Sioi juzi na jana, alidai kwamba Dk Slaa anawajibika kuwajibu Watanzania sababu za kufukuzwa kwake ukasisi ndani ya Kanisa Katoliki, kabla ya kuingia kwenye siasa.

Wassira alisema Dk Slaa ambaye amekuwa msitari wa mbele kukemea ufisadi nchini, si mkweli kwani alifukuzwa baada ya kutafuna fedha za ujio wa Papa John Paul – II aliyezuru Tanzania mwaka 1990, wakati huo Slaa akiwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

“Huyu Dk Slaa alitafuna fedha za ujio wa Papa miaka ya nyuma na ndio chanzo cha kufukuzwa upadri,tena haya hata nyie mlichanga hizo fedha kwenye vigango vya parokia si mnakumbuka,”alisema Wassira.

Wassira aliendelea kumtuhumu Dk Slaa kwamba anaendeleza ufisadi ndani ya Chadema kwa kile alichodai kwamba alimfukuza kazi mhasibu wa chama hicho, kwa kosa la kushindwa kumlipa mchumba wa Dk Slaa, Josephine Mushumbusi kiasi cha Sh10 milioni.

Wakati huo huo,Wassira ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema kwamba mgombea ubunge wa Chadema,Joshua Nassari hafai kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa ni kijana mkorofi na mara kwa mara, baba yake mzazi amekuwa akimsihi kuachana na ukorofi tangu wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema kwamba baba wa mgombea huyo ambaye ni kiongozi wa dini, amekuwa akimsihi kuachana na ukorofi ikiwa ni pamoja na kuoa ili aweze kutulia lakini cha ajabu, Nassari amekuwa akionekana na bibi wa kizungu mwenye umri wa zaidi ya miaka 60 akizunguka naye mitaani jijini Arusha.

Wakati Wassira akitoa kauli hiyo, baba yake Nassari, Mchungaji Samuel Nassari na mkewe walihudhuria uzinduzi wa kampeni za mtoto wao zilizofanyika Jumamosi ya wiki jana kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Leganga, Usa River.

Chadema na rada
Katika mikutano yao juzi na jana, Chadema kwa upande wake walitaka kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani, wahusika wote wa ufisadi wa rada.

Meneja mwenza wa Kampeni za chama hicho jimboni Arumeru Mashariki, Vincent Nyerere, akizungumzia kurejeshwa kwa fedha za rada, alisema hoja sio kufurahia bali ni kuwafikisha mahakamani wote waliohusika na kununua rada kwa ulaghai, hivyo kujipatia mabilioni ya fedha.

“Hoja hapa sio kurejesha chenji eti zinunuwe madawati na vitabu, hoja ni hatua gani wanachukuliwa waliohusika na kununua rada ili kujipatia fedha ambazo zilisababisha watoto wao kusoma nje na watoto wa masikini kufa kwa kukosa madawa hospitali na kukaa chini?,”Alihoji Nyerere ambaye ni Mbunge wa Musoma Mjini.

Alisema ikiwa Serikali haitawakamata watuhumiwa wa ufisadi huo, basi wafungwa wote waliotiwa hatiana kwa makosa madogo madogo kama kuiba kuku, waachiwe.

Mbunge huyo pia alimgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kwa kusema kwamba kiongozi huyo hana mamlaka ya kumzuia kumzungumzia baba yake,Hayati Julius Nyerere jukwaani kwani yeye si mwanafamilia bali ni msajili wa vyama.

Akizungumza katika mikutano iliyofanyika katika vijiji cha Ngarenanyuki na Msitu wa Tembo, Nyerere alisema Tendwa kama anataka awe mwanafamilia wa Nyerere kwa kuomba, afanye hivyo.

“Tendwa ni Msajili wa Vyama vya Siasa sio msajili wa koo, kama kazi ya siasa imemshinda basi awe msajili wa koo,”alisema Nyerere.

Mbunge huyo alisema alilazimika kutoa kauli nzito dhidi ya Mkapa baada ya kutoa taarifa ya uongo kuwa hamtambui kama mwanaukoo wa Nyerere.

Akizungumzia hoja ya Tendwa kuwa wakati wa kifo cha Mwalimu, yeye (Vincent) alikuwa mtoto, alimtaka Tendwa afanye uchunguzi na kuuliza wengine kwani yeye hakuwa mtoto wakati wa kifo cha Mwalimu na kwamba alikuwa na ufahamu wa kila kilichotokea wakati huo.

Ahadi za wagombea
Wakati viongozi wa Chadema na CCM wakiendelea kupimana ubavu majukwaani, wagombea wao Nassari na Sioi, sawia wameendelea kutoa ahadi za kutatua kero za wakazi wa Arumeru Mashariki ambao kilio chao kikubwa ni uhaba wa ardhi na maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na umwagiliaji mashamba.

Nassari katika ahadi zake juzi na jana alisema ikiwa atachaguliwa kuwa mbuge, atapeleka hoja binafsi bungeni kudai ardhi ya Meru ambayo kwa sehemu kubwa ipo mikononi mwa walowezi wachache.

Alisema zaidi ya ekari 13,000 zinamilikiwa na watu wachache ambao wameanzisha mashamba ya maua na kujenga viwanja vya gofu na farasi, huku wakizuia maji kufika katika makazi ya watu na badala yake maji hayo, kutumika kumwagilia uwanja na kuogeshea farasi.

CHANZO: Mwananchi, kusoma zaidi habari hii BOFYA; http://www.mwananchi.co.tz/