SEMINA elekezi kwa ajili ya mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 itafanyika Machi 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo washiriki ni makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa au wawakilishi wao ambao wanatakiwa kuwa na utambulisho rasmi.
Washiriki kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam wanatakiwa kuwasili Machi 24 mwaka huu na watapokelewa katika hoteli ya Itumbi iliyoko Magomeni-Mwembechai. TFF itawagharamia washiriki kwa chakula, malazi na nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa usafiri wa basi au meli.
Michuano ya mwaka huu itaanza Machi 31 hadi Mei 5 katika ngazi ya wilaya. Usajili kwa ngazi ya mkoa utaanza Mei 6 hadi 15 wakati mashindano yake yatafanyika kuanzia Mei 16 hadi 25.
Usajili na maandalizi kwa michuano ya ngazi ya Taifa utaanza Mei 26 hadi Juni 7. Usajili wa timu za mikoa unatakiwa kuwasilishwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kati ya Juni 8 na 14 mwaka huu.