JK amkumbuka marehemu Salum Amour Mtondoo

Marehemu, Salum Amour Mtondoo

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kuomboleza kifo cha Mwakilishi wa Jimbo la Bububu (CCM) Salum Amour Mtondoo.
Hayati Mtondoo alizikwa kijijini kwao Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja Machi 16, 2012, baada ya kufariki dunia juzi kwa matatizo ya shinikizo la damu, malaria na sukari.
Katika salamu zake kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa mshtuko na masikitiko habari za kifo cha Mheshimiwa Mtondoo ambaye alikuwa Mwakilishi wa Wananchi wa Bububu katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko habari za kifo cha Mheshimiwa Mtondoo. Siyo tu alikuwa mwanachama hodari wa chama chetu, lakini pia katika kipindi chake cha uwakilishi amefanya kazi nzuri na ya kukumbukwa ya kutetea ipasavyo maslahi ya wananchi wa jimbo lake kwa uadilifu na moyo mkubwa wa kujituma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kupitia kwako Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa Wawakilishi wote kwa kuondokewa na wenzao, kwa wananchi wa Bububu kwa kumpoteza mwakilishi wao hodari na kwa wana-CCM wa jimbo hilo kwa kifo cha mwanachama mwenzetu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, naomba uniwasilishie salamu zangu kwa wanafamilia wote wa Mtondoo kwa kupotelewa na mhimili mkuu wa familia. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Aidha, nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amen.”