Na Mwandishi Wetu, Rukwa
WATU wanaosadikiwa kuwa Majambazi juzi usiku walifanya kufuru jirani na nyumbani kwa wazazi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda eneo l kibaoni Kata ya Usevya tarafa ya Mpibwe wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, baada ya kuvamia nyumbani kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibaoni, LADSLAUS MUNGUWAJUA (37)
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Jacob Mwaruanda amesema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tatu usiku, majambazi hao walikuwa wanne wakiwa na bunduki isiyojulikana na marungu walivamia nyumba hiyo na kuanza kumshambulia Mtendaji huyo kichwani kwa kutumia marungu na kumlazimisha
awapatie fedha.
Majamabazi hao walifanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha sh. milioni moja ambayo ni mali ya Mtendaji huyo, ambae ujishughulisha na biashara, huku yakimlazimisha kuwapatia funguo za kasiki (SAFE) walilolikuta nyumbani kwa
Mtendaji ambalo hulitumia kuweka fedha anazozipata katika biashara ya kuuza mabati kwa bei ya punguzo. Inasemekana mabati hayo ni ya kampeni ya Ondoa nyasi mkoa wa Rukwa maarufu kwa jina la ONYARU, inayofanyika katika mikoa ya Rukwa na Katavi mradi ambao inasemekana ni juhudi za Waziri Pinda.
Hata hivyo Mtendaji huyo baada ya kubanwa na kupigwa bado alikana kuwa hana funguo ya kasiki hilo kwa sababu zilikuwa tayari zimepotea siku tatu kabla ya tukio hilo ambalo nalo walijaribu kulifungua kwa kutumia silaha zao na kushindwa kabisa na kuamua kuondoka na kuliacha pale pale.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa na Katavi, Jacob Mwaruanda majambazi hao walimjeruhi pia Mwenyekiti wa kijiji hicho, Gaston Kamina miaka (52) ambae alikutwa pale akiangalia video na kujeruhiwa mkononi kwa marungu ambapo alitibiwa zahanati ya kijiji hicho na kuruhusiwa.
Mtendaji huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambapo alitibiwa na kuruhusiwa Polisi walifika eneo la tukio usiku huo na kuendesha msako ambapo waliwakamata watuhumiwa wawili WILEMBO SALUM miaka (35) na KHERI OBEID Miaka (30) wote wakulima wa kijiji jirani cha Usevya.
Mwaruanda alisema eneo la tukio kuliokotwa maganda mawili ya risasi za SMG/SAR watuhumiwa hao bado wanahojiwa na watafikishwa mahakamani hivi karibuni mara baada ya uchunguzi wa awali utakapokamilika.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika na uvamizi huo.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya amemwagiza Kaimu Kamanda huyo kuhakikisha anashiriki katika kuwasaka wote walioshiriki kuvamia kijiji hicho anachotoka Waziri Mkuu Pinda. Manyanya alisema ni lazima watuhumiwa hao wafikishwe katika sheria na kutoa onyo kwa wengine wanaodhani mikoa hiyo ni kimbilio la waharifu.
MWISHO.