Serikali yaanza kuvitwaa viwanda vilivyotelekezwa

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WIZARA ya Viwanda na Biashara imeanza mchakato wa kufuatilia viwanda 15 vilivyokufa toka kwa wawekezaji ili kuvunja mikataba yao na kuwapa wawekezaji wenye uwezo ambao wataviendeleza kwa lengo la kuinua uchumi wa Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa mjini hapa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami wakati akizungumza na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Moshi vijijini na watendaji wa kiwanda cha sukari cha TPC ambapo madiwani walitembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea hali halisi ya utendaji kazi wake.

Viwanda hivyo 15 ni kati ya viwanda 74 vilivyopo chini ya wizara ya
viwanda na biashara vilivyobinafsishwa kabla ya kufa kutokana na sababu anuai ikiwemo mitaji midogo na kutokuwa na teknolojia mpya na za kisasa.

Dk. Chami alisema Kwa sasa shirika Hodhi la mali za taifa linaendelea
na mazungumzo na wawekezaji wa viwanda hivyo 15 ambavyo vimekufa ili kuangalia uwezekano wa kuvunja mikataba na kuvikabidhi kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendeleza.

“Serikali haiwezi kukaa kimya kuviangalia viwanda hivi ambavyo
vimeshindwa kuendelea, inafanya utaratibu wa kuvirudisha mikononi mwa Serikali kwa kufuata utaratibu na kuwapa wawekezaji wengine wenye uwezo ili wavifufue na kufanikisha malengo ya serikali ya kukuza soko la ajira hapa nchini,” alisema Dk. Chami.

Dk. Chami alifafanua kuwa serikali ilibinafsisha viwanda 74 na kai ya
hivyo 42 vinafanya kazi nzuri na kupita malengo waliyokubaliana na
serikali, 17 vinafanya kazi kwa kusuasua huku 15 vikishindwa kabisa
kuendelea.

Alisema nia ya serikali kuvibinafsisha viwanda ilikuwa njema na ni ili
kuinua uchumi wa nchi na soko la ajira lakini kufa kwa viwanda hivyo
kumepelekea malengo na nia njema ya serikali kushindwa kufanikiwa.

Aidha alisema pamoja na hali hiyo kwa sasa serikali inashirikiana na
wawekezaji wa viwanda 17 ambavyo utendaji kazi wake si wa kuridhisha
ili kuangalia uwezekano wa kuviboresha na kulinda soko la ajira na
huduma nyingine za kijamii.

“Pamoja na viwanda 15 kufa pia viko vingine 17 ambavyo vina matatizo
ya hapa na pale kama vile upatikanaji wa malighafi na kubadilika kwa
masoko, lakini vipo viwanda 42 ambavyo kwa kweli vinafanya kazi nzuri
na vimeweza kuvuka lengo walilokubaliana na Serikali kikiwemo kiwanda
cha sukari cha TPC ambacho lengo la serikali ni kufikia uzalishaji wa
Tani 72,000 lakini chenyewe kwa sasa kinazalisha sukari tani
85,000,” alisema Dk. Chami.

Akizungumza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, Robert Baissac, alisema wakati kiwanda hicho kinabinafsishwa kilikuwa kinazalisha sukari tani 36,000 na kutakiwa kuongeza usalishaji marambili hadi kufikia tani 72,000 lakini wameweza kuvuka lengo hilo na kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 85,000 kwa mwaka.

Awali akizungumza Ofisa Utawala Mkuu wa kiwanda cha TPC, Jafary Ally alisema kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, uhaba wa ardhi, tatizo la maji ambapo maji mengi yanayopatikana kiwandani hapo yana magadi.

Alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa magadi katika maeneo ya kiwanda hivyo kusababisha kutumia gharama kubwa kuondoa magadi hayo pamoja na uvamizi wa eneo la kiwanda unaofanywa na wananchi mbalimbali wanaozunguka kiwanda hicho.