Nitawaacha Watanzania wenye afya njema-Rais Kikwete

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Rais wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno nchini, Dk. Rachel Mhavile (kulia) na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donnan Mmbando baada ya kufungua mkutano wa siku tatu wa kujadili jinsi ya kuyaweka masuala ya kinywa na meno katika hatua ya awali ya kupata huduma ambapo jumla ya wajumbe kutoka nchi 18 wanahudhuria mkutano huo. Picha na Anna Nkinda - Maelezo.

Na Magreth Kinabo–MAELEZO

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Serikali yake itafanya kila iwezavyo kuhakikisha inanatoa huduma bora za afya na za kisasa ili taifa liwe na watu wenye afya njema, ikiwa ni pamoja na kuzuia na kutibu magonjwa anuai katika kipindi cha uongozi wake.

Kauli hiyo imetolewa jana na Rais Kikwete mara baada ya kukabidhiwa kadi, katiba na tuzo ya kukubali kuwa mwanachama wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania iliyotolewa na Rais wa chama hicho, Rachel Mhaville jijini Dar es Salaam.

“Sikutegemea kutokea kwa kitendo hiki. Ninachoweza kusema ninaomba mniamini nitakuwa mwanachama mzuri. Tutafanyakazi kwa pamoja ili kutimiza ndoto zenu hususan kuhakikisha mradi wa kituo cha Kigamboni cha magonjwa hayo unaanzishwa. Hili ni jukumu kwangu, kwani lengo langu ni kuliacha taifa likiwa lenye watu wenye afya njema,” alisema Rais Kikwete.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisoma jarida la Meno Tanzania alilokabidhiwa na Rais wa chama cha madaktari wa Kinywa na Meno Dk. Rachel Mhavile mara baada ya kufungua mkutano wa siku tatu wa kujadili jinsi ya kuyaweka masuala ya kinywa na meno katika hatua ya awali ya kupata huduma . Jumla ya wajumbe kutoka nchi 18 wanahudhuria mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam.


Aliongeza kuwa Serikali yake inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha ujenzi wa Chuo Kikuu kipya cha Sayansi za Afya na Tiba eneo la Mlongazila unafanikiwa ili kiweze kufanya kazi kabla ya mwaka 2015. Rais Kikwete alisema chuo hicho kitakuwa na shule mbalimbali za afya na tiba.

Akifungua mkutano wa mafunzo ya siku tatu ya kuweka hatua za awali za kupata huduma za kuzuia na kutibu magonjwa hayo, Rais Kikwete alisema bado kuna safari ndefu ya kuiwezesha sekta ya huduma hiyo kuwa na rasimali watu wa kutosha wakiwemo madaktari, wauuguzi na watumishi wengine wa eneo hilo.

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka nchi 18 wanahudhuria mkutano wa siku tatu wa kujadili jinsi ya kuyaweka masuala ya kinywa na meno katika hatua ya awali ya kupata huduma unaofanyika jijini Dar es Salaam (Picha zote na Anna Nkinda-Maelezo)


Rais Kikwete aliongeza kuwa sekta hiyo ina upungufu wa madakatari ukilinganisha na idadi ya watu nchini wapatao milioni 43 .

Alizitaja takwimu za madaktari wa sekta hiyo nchini kuwa wapo 518 ambapo uwiano unaonesha kuwa 1: 120,000 (yaani daktari mmoja kwa wagonjwa 120,000) wakati kwa sheria za Shirika la Afya la Dunia (WHO) 1:7500 (yaani daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 7500).

“Serikali itaendelea kujenga uwezo kwenye hospitali na kituo cha afya, lazima ziwe na vitengo vya huduma za kinywa na meno,” alisisitiza huku akiongeza kwamba itasaidia kuanzisha na kupanunua vilivyopo na itangalia ili iweze kuanzisha hata katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Alitoa changamoto kwa wadau wa sekta hiyo kuhakikisha kuwa huduma za magonjwa hayo zinapatiakana, kutolewa katika hatua za awali na kwa gharama nafuu.

Naye Rais wa chama hicho, Mhaville alisema aliitaka jamii kuacha kutembea na magonjwa hayo badala yake wafike hospitali ili kupata ushauri na tiba kwa kuwa magonjwa hayo yanazuilika. Alisema changamoto iliyopo kwao ni kutoa elimu kwa jamii hususan kwenye maeneo ya vijijini. Mhaville alisema mkutano huo utatengeneza mwongozo wa mamna ya kuyashughulikia magonjwa ya afya ya kinywa na meno, ambapo Rais alisema Serikali inausubiri kwa hamu.