Serengeti Breweries yatoa mil 10.92 kuwazawadia waandishi wa habari

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa SBL, Bi. Teddy Mapunda (katikati) akimkabidhi mfano wa hundi ya sh. 10,925,000 Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga (wa pili kushoto). Wengine kutoka kulia ni Meneja Mawasiliano wa SBL, Iman Lwinga, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda na Meneja wa Miradi ya Jamii SBL, Nandi Mwiyombella.

Na Joachim Mushi

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imetoa jumla ya sh. milioni 10,925,000 fedha ambazo zitatumika kuwazawadia waandishi wa habari ambao watashinda katika uandishi bora wa habari eneo la Utawala Bora.

Fedha hizo zimekabidhiwa leo jijini Dar es Salaam kwa waandaaji wa tuzo hizo ambao ni Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakiwa na lengo la kuwasaka waandishi bora katika uandishi wa habari maeneo tofauti kuchochea uandishi wa habari unaofuata maadili.

Akikabidhi mfano wa hudi ya kiasi hicho cha fedha Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa SBL, Bi. Teddy Mapunda amesema kampuni hiyo imeamua kutoa mchango huo ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa wanahabari na kuchochea uandishi wa maadili nchini.

Alisema SBL inatambua kuwa utoaji wa tuzo kwa wanahabari unaleta changamoto na kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao jambo ambalo pia litachangia maendeleo ya taifa katika sekta mbalimbali.

“Tunathamini mchango mzima wa sekta ya habari na waandishi wenyewe, tumekuwa tukishirikiana nao vizuri katika utendaji wa majukumu yao. Tuzo kama hizi kwa wanahabari zinaleta motisha na changamoto kwa wanahabari na ndiyo maana tumeamua kutoa mchango wetu…,” alisema Mapunda.

Aidha SBL pia imetoa mchango wa masanduku 40 ya bia pamoja na katoni kadhaa za vinywaji vikali aina ya ‘John Walker’ ambavyo vitatumika katika hafla maalumu ya kuwazawadia waandishi bora inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Naye Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga akizungumza baada ya kupokea mfano huo wa hundi kutoka SBL, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wadau wa sekta ya habari ikiwemo MCT.

Mukajanga alisema SBL imekuwa ikisaidia masuala mbalimbali kiudhamini kwa kushirikiana na MCT tangua mwaka 2009 tulipoanza mchakato huu. “Kweli SBL tunawashukuru maana wamekuwa wakitusapoti tangu mwaka 2009…,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Aliongeza kuwa mbali na mchango huo, SBL walidhamini tuzo za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) mwaka jana kwa takribani milioni 100 pamoja na semina ya wahariri iliyofanyika mkoani Arusha.

Hafla hiyo ya makabidhiano ya kiasi hicho cha fedha pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absolom Kibanda, ambao ndiyo walioishawishi SBL kuchangia tuzo za uandishi bora za mwaka huu eneo la utawala bora, Kamati ya Tuzo za Waandishi Bora za mwaka huu pamoja na wanahabari.