Na Mwandishi Wetu
UJUMBE wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), uliokuwa ukifanya tathmini ya hali ya uchumi na fedha nchini, umesema Tanzania inafanya vizuri kiuchumi licha ya matatizo kadhaa ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi yanaolikabili taifa.
Ujumbe huo uliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa umeme wa uhakika kulikotokana na ukame uliotokea mwaka 2011 na kuathiri shughuli za uzalishaji mali viwandani na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia.
Kauli hiyo imetolewa jana kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Wajumbe hao, Peter Alumu ambaye pia ni Mshauri wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), anayeshughulikia masuala ya Afrika. Kiongozi huyo amesema tathmini waliyoifanya imeonesha uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia 6.3 katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka 2011.
Amesema dalili zinaonesha kuwa mfumuko wa bei umepungua kwa asilimia 19.8 (mwaka 2011) hadi chini ya asilimia 10 na endapo uzalishaji viwandani utaongezeka sambamba na kufanya vizuri kwenye kilimo, mwaka 2012 mfumuko utapungua zaidi.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu amesema shirika hilo limeshauri Serikali kuboresha kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuwa makini katika matumizi yake. Katika hatua nyingine Serikali imeshauriwa kuwa na mpango wa mkopo wa dharura kutoka shirika hilo ili kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi endepo utatokea.