WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezitaka kampuni na taasisi zinazohusika na kutoa huduma muhimu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwl. Julius Kambarage Nyerere ziharakishe kufanya hivyo ili ujenzi wake ukamilike mapema.
Ametoa kauli hiyo Jumamosi ya Machi 10, 2012 mara bada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kituo hicho na kukagua ujenzi wake katika mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam.
Kampuni zinazotakiwa kufanya hivyo ni TANESCO kwa ajili ya umeme wa jengo hilo, Kampuni ya Simu (TTCL) kwa ajili ya mkonga wa mawasiliano na Idara ya Kodi ya Mapato (TRA).
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha mikutano ni ishara ya urafiki wa muda mrefu ulikuwepo baina ya Tanzania na China na kwamba kukamilika kwake kutaboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo ambalo litagharimu yen milioni 183.5 sawa na dola za Marekani milioni 30, Balozi wa China nchini Tanzania, Bw. Lv Youqing alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mara baada ya sherehe za uzinduzi Januari 15, 2010.
Awali, ujenzi wa jengo hilo ulitarajiwa kukamilika Aprili, 2012 lakini kutokana na uchelewashaji wa miundombinu hiyo muhimu hivi sasa linatarajiwa kukamilika Agosti, mwaka huu.
Litakapokamilika jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 1,000; litakuwa na kumbi ndogo ndogo nne zenye uwezo wa watu zaidi ya 20, ukumbi wa chakula wa watu zaidi ya 700 na ofisi za watumishi wa ukumbi huo. Vilevile, kutakuwa na ukumbi mmoja ambao unaweza kugawanywa (partitioned) na kutengeneza ofisi za muda kwa watu wanaoendesha mkutano mkubwa katika ukumbi huo.
Naye Mkurugenzi wa mradi wa ujenzi wa kituo hicho, Bw. Huang Meiluan alisema ujenzi wa ghorofa ya chini umekamilika kwa asilimia 40 kwa sababu bado wanasubiri huduma muhimu zikamilike ili waanze kuweka sakafu. “Tunasubiri kuunganishwa na mkonga wa mawasiliano wa Taifa, bado hatujaweka njia kuu za umeme za kuingia katika jengo… kasi ya ujenzi imeathirika kutokana na kutokamilika kwa huduma hizi muhimu,” alisema.
Alisema ujenzi wa ghorofa ya kwanza na ya pili umekamilika kwa asilimia 90 na imebakia kazi ya kumalizia kuweka nakshi za ndani tu (interior decoration). “Kwa nje, kazi ya ujenzi imekamilika na tumeanza kuweka nakshi, kazi hii imekamilika kwa asilimia 75,” alisema.
Alisema wanakabiliwa na changamoto ya wizi wa vifaa vya ujenzi unaofanywa na vibaka kila mara na kwamba inawapa mtihani kwani itawalazimu kuagiza upya vifaa hivyo kutoka China. Aliomba polisi wawasaidie kuimarisha ulinzi katika eneo la ujenzi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imeanza kushughulikia upatikanaji wa kifaa muhimu cha umeme ambacho kilishindwa kupatikana hapa nchini.
Alisema vyuma vilivyotumika katika hatua za awali za ujenzi wa kituo hicho ni tani nyingi, na kwamba yanahitajika malori ya kuvisomba na kibali kutoka TRA ili yaweze kupelekwa katika eneo jingine kwa kuhifadhiwa. Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba wizara yake inafuatilia suala hilo pia.
Kuhusu uwekwaji wa nyaya za mkonga wa mawasiliano ambao unapaswa kufanya na TTCL, waziri Membe aliomba apewe wiki moja zaidi kwani amekuwa akisumbuana nao kwa zaidi ya mwezi mmoja bila mafanikio yoyote. Suala la ulinzi pia alisema ameshaanza kulishughulikia.