MADAKTARI nchini Tanzania wamesitisha mgomo wao mara moja ikiwa ni baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na kuwasilisha madai yao, huku akiahidi kuyafanyia kazi madai hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo mtandao huu umeipata kutoka kwa Jumuiya ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), imeeleza kuwa wamefikia hatua hiyo ya kusitisha mgomo baada ya kukutana na Rais Kikwete jana Ikulu.
Taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amepokea hoja za madaktari na kuahidi kuzifanyia kazi. “Tulikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MH. DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE. Tulimweleza hoja zetu ambazo amezielewa na kuahidi kuzishughulikia kikamilifu. Tunaimani sana na MH. RAIS kwamba hatatuangusha.
“Kutokana na hilo tunapenda kuutangazia umma wa Watanzania kuwa tunarudi kazini rasmi kuanzia Machi 10, 2012, Wakati Mheshimiwa Rais akishughulikia madai yetu,” imesema taarifa hiyo ya MAT.
Hata hivyo katika taarifa hiyo MAT wameeleza wazi wazi kuwa hawana imani na WAZIRI WA AFYA MH. DR. HAJI MPONDA pamoja na Naibu wake MH. DR. LUCY NKYA, na kuwa wamemsimamisha uanachama wa MAT MH. DR. LUCY NKYA.
“Madaktari tunatamka wazi kuwa Waziri wa Afya DR. HAJI MPONDA na Naibu wake DR. LUCY NKYA ni maadui wa madaktari na sekta ya afya kwa ujumla hapa nchini na tunaahidi kutowapa ushirikiano wa aina yoyote wa kibinafsi au wa kiutendaji,” imesema taarifa hiyo.
Pamoja na kutoa tamko hilo pia MAT imetoa ufafanuzi juu ya mgomo wao ikisema kuwa;- kwanza Jamii ielewe kuwa daktari kama binadamu mwingine anayefanya kazi Tanzania ana mahitaji muhimu (basic needs) na mahitaji ya kijamii (social responsibility) na hivyo si chombo cha kufanyia kazi (Machine).
na pili, pia Daktari ana haki ya kupata ujira unaomfaa kutokana na kazi anayofanya na ana haki ya kuacha kazi muda wowote iwapo ataona kazi hiyo ya udaktari haimpi ujira wa kutosha na heshima ya kuendesha maisha yake.
Tatu, jamii itambue kuwa daktari anaweza kulazimishwa kurudi kazini lakini hawezi kulazimishwa kufanya kazi. Matokeo ya kulazimishwa yanaweza yasiwe mazuri kwa wale watakao hudumiwa na nne, jamii itambue kuwa madai na hoja kuu za madaktari ni kwa ajili ya faida ya Watanzania wote, yakiwemo mazingira bora ya kufanya kazi mjini na vijijini, na kuboresha afya za watanzania kwa ujumla. Pia vifaa na dawa ziwepo mahospitalini zinakohitajika.
Na mwisho MAT imewashukuru madaktari wote kwa mshikamano wetu tulioonyesha na tunaomba mshikamano huu uendelee daima.