Na Joyce Ngowi
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) wamesitisha mgomo baada ya Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu kusikiliza kilio chao sugu kwa miaka 10.
Kauli hiyo ya kusitisha mgomo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Erasto Kihwele. Akifafanua zaidi alisema wamesitisha mgomo baada ya kukutana na Waziri wa Uchukuzi na kusikiliza madai yao ya mishahara na mafuta ambayo yamekuwa matatizo sugu kwa miaka 10.
Katibu huyo alisema waligoma kwa kuzingatia usalama wa wananchi wanaosafiri kwa njia ya reli ambapo walikuwa wakihofia kushindwa kumaliza safari kutokana na mafuta yanayotolewa kuwa kidogo pia kukosa mafuta ya akiba kwa ajili ya dharura kwani iwapo treni ingeharibika ikiwa njiani inge kuwa ni hatari kubwa kwa wasafiri.
“Hoja ya msingi ni mishahara ambayo baadhi ya wafanyakazi hawajalipwa kwa miezi miwili hali inayofanya maisha yao kuwa magumu pia kushindwa kutimiza wajibu wa kazi katika shirika hilo,” alisema kiongozi huyo.
Aidha akifafanua juu ya tuhuma za uuzwaji wa vichwa viwili vya treni alieleza kuwa bado wanafuatilia kwa ukaribu taarifa ya kuuzwa kwa vichwa hivyo ili kuweza kubaini mazingira yaliyotumika kuhalalisha uuzwaji wa vichwa hivyo.
Aliongeza kuwa kama hujuma hiyo itabainika basi watu ambao wamehusika kuuza vichwa hivyo lazima wachukuliwe hatua kwa lengo la kukomesha tabia ya ubadhirifu wa mali za umma. Alisema madai mengine ni kupeleka vielelezo kwa Waziri wa Uchukuzi vya ubadhirifu unaofanywa na mameneja wa Tazara hali ambayo inafanya shirika hilo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na mazingira hayo ya ubadhirifu.
Mwanzoni mwa wiki hii wafanyakazi wa Tazara waligoma kusafirisha abiria jambo lililosababisha abiria kulala kituono hapo na baadaye kurejeshewa nauli zao, jambo hilo lilikuwa zito kwa wasafiri waliokuwa wakisafirisha maiti za ndugu zao kuelekea mkoani Morogoro