Na Aron Msigwa – MAELEZO
SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara ya nchi hiyo imeandaa maonesho makubwa ya bidhaa zinazozalishwa na kutengenezwa nchini China, ambayo yatafanyika barani Afrika kwa lengo la kuinua na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kwa mataifa ya Afrika.
Akizungumza na wadau wa biashara kutoka China na Tanzania jijini Dar es salaam jana Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya nchi za nje kutoka Wizara ya Biashara, Bi. Xiao LU amesema maonesho hayo mwaka huu yatafanyika nchini Tanzania kutokana na uhusiano mzuri wa kibiashara uliopo baina ya mataifa haya.
Amesema Tanzania ni moja ya eneo muhimu kibiashara katika Afrika Mashariki linalozungukwa na nchi za Ethiopia, Kenya, Msumbiji, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ameongeza kuwa bidhaa za China zinatambulika duniani kote kutokana na upatikanaji wake, bei nzuri na ubora wake huku akifafanua kuwa nchi hiyo kutokana na maendeleo ya kiteknolojia imejipanga kudhibiti bidhaa feki.
“Hivi sasa bidhaa zetu zinatambulika dunia nzima kutokana na ubora mzuri zilizonao pamoja na bei nzuri, kwa maendeleo makubwa ya teknolojia tuliyonayo tumekuwa tukiongeza ubora wa bidhaa zetu kimataifa” amesema Bi. LU.
Ameongeza kuwa maonesho hayo yatawashirikisha wafanyabishara wakubwa na wadogo yakihusisha bidhaa anuai kutoka China zikiwemo bidhaa za vyakula, magari, mitambo ya viwandani na kilimo, vifaa vya umeme, vifaa vya mawasiliano, vifaa vya ujenzi pamoja na bidhaa nyingine nyingi yamelenga kuinua na kuimarisha ushirikiano kibiashara kutokana na mabadiliko ya uwekezaji na mabadiliko ya uchumi yanayotokea duniani.
Mbali na bidhaa hizo zitakazoonyweshwa Bi. LU amesema maonyesho hayo yataimarisha ushirikiano wa kiutamadauni baini ya Tanzania na China na nchi nyingine za Afrika ya mashariki. Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda nchini Tanzania (TCCIA), Aloys Mwamanga amesema maonyesho hayo ni changamoto kwa wafanyabishara, wakulima na wenye viwanda wa Tanzania kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa zao ili waweze kusafirisha bidhaa nyingi zaidi kwenda nchini China na kuongeza pato la Taifa.
Pia ametoa wito kwa washiriki hao kutoka nchini China kujikita katika kuonyesha bidhaa za uzalishaji zinazoweza kuongeza thamani ya mazao zikiwemo bidhaa za kilimo na kuwataka kuongeza juhudi ya upambanaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.