Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal amesema ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015 mkazo mkubwa utawekwa katika sekta ya afya ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
Akifungua kongamano la siku mbili la kimataifa kuhusu utendaji bora katika huduma za afya (malipo kwa ufanisi) Dk. Bilal amesema wizara ya afya nayo itatakiwa kufuata utaratibu huo ambao kwa sasa umeanziashwa na tume ya kikristo ya huduma za jamii (CSSC) ili kuboresha sekta ya afya.
Utaratibu wa malipo kwa ufanisi katika sekta ya afya umeanzwa kutekelezwa katika nchi saba barani Afrika ambapo hapa nchini unatekelezwa katika wilaya ya rungwe mkoani mbeya.
Nchi hizo zinazohudhuria kongamano hilo ni Rwanda,Congo, Burundi, Zambia,Tanzania,Cameroon na Jamhuri ya Africa ya Kati na afghanstan lengo likiwa kuongeza motisha kwa watumishi wa sekta ya afya ili kulinda uhai wa wanadamu.
Rais wa CSSC Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mwanza Jode Thaddeus Ruwaichi amesema mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika wilaya ya rungwe umeonesha mafanikio mengi na hivyo utaendelezwa katika maeneo mengi nchini ili kuleta tija na ufanisi katika ustawi wa maisha ya watu hususan maskini na wasiojiweza.
Ameitaka serikali kutekeleza mpango huo katika hospitali zake kwa kuunda sera itakayoongoza mpango huo ili kuwezesha sekta ya afya kufanyakazi kwa ufanisi.
Nae Mkurugenzi wa CSSC Bwana, Peter Maduki amesema kongamano hilo la siku mbili linalokutanisha wadau wa afya kutoka nchi mbalimbali Afrika na Afghanistan ni fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu mpango wa malipo kwa ufanisi, kuunda mtandao wa kimataifa kuhusu sekta ya afya na kuchochea ushirikishwaji wa jamii katika mifumo mwili ya ugharimiaji wa huduma za afya, malipo kwa ufanisi na bima ya afya.
Tume ya kikristo ya huduma za jamii CSSC ni chombo cha pamoja cha makanisa kilichoanzishwa na baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), na jumuiya ya kikristo Tanzania (CCT), mwaka 1992, lengo likiwa ni kuratibu huduma za kijamii zinazotolewa na makanisa wanachama hususan huduma za afya na elimu.