Mchungaji ataka Tanzania iombewe

Bendera ya Tanzania

WATANZANIA wametakiwa kuiombea nchi yao ili iweze kudumu kuwa nchi ya amani na iendelee kustawi kiuchumi. Wito huo umetolewa Machi 4, 2012 na Mchungaji Tumaini Mwanyonga wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Ilala wakati akihutubia kwenye ibada ya kuhitimisha maombi ya wiki nzima ya Wanawake Watumishi wa Kristo (WWK) kwenye kanisa la TAG Mwenge jijini Dar es Salaam.

WWK ni chama cha akinamama wa Kanisa la TAG ambalo kila mwaka huweka siku maalum ya akinamama kuadhimisha siku yao. Mwaka huu ilipangwa kuwa Machi 4, 2012 na maadhimisho yake yalianza Februari 27, mwaka huu.

Katika mahubiri yake, Mch. Mwanyonga alisema Tanzania imegubikwa na migomo ya wanafunzi, migogoro ya madaktari, kushuka kwa uchumi, kuporomoka kila mara kwa thamani ya shilingi, kudumaa kwa hali za uchumi katika baadhi ya mikoa, mambo ambayo alisema hayaleti amani na furaha kwa Watanzania.

“Tunapaswa kusimama imara na kuliombea Taifa letu ili uchumi usiendelee kuyumba wala thamani ya shilingi isiendelee kushuka, tunapaswa kuliombea Taifa katika mipango yake ya bajeti, tunapaswa kulikomboa Taifa hili na migogoro ya kila mara…tukiacha hali hii iendelee hatuna Tanzania itakayoendelea, hatuna kanisa litakalozalishwa hapa nchini,” alisema.

Alisema kushindwa kufanya mambo siyo kuharibikiwa; lakini kama Taifa, wanahitajika watu ambao wataibaini hali hiyo na kusimama katika nafasi zao na kuomba kwa nguvu ili Mungu aweze kuleta njia ya kuondokana na hali hiyo.

“Tunahitaji watu ambao wanaweza kuthubutu, watu ambao wanaweza kuingiza miguu yao katika maji yenye kina na kusonga mbele huku wakiamini kwamba huko mbele kuna upenyo,” aliongeza.

Alisema kila mmoja ana nafasi ya kuiombea nchi ya Tanzania na kuiponya kama kweli atadhamiria kufanya hivyo. “Kila mmoja aseme nataka kuona uharibifu ukiondoka katika nchi ya Tanzania, kila mmoja aseme nataka kuona dhambi ikiondoka katika nchi yetu…hakuna kuchoka wakati tunatembea katika maombi,” alisisitiza.

Alisema kama watajitokeza watu waaminio ambao watakiri nguvu na mamlaka ya Mungu, wakaikubali, wakaipenda na kuitumia nguvu hiyo, watagundua jinsi ambavyo Mungu atafanya mambo magumu yawe mepesi.

“Katika maombi hakuna kukata tamaa, kwa sababu katika dakika za mwisho ndipo Mungu huwa anajibu. Tuingie katika maombi ya Taifa iwe ni katika masuala ya uchumi wa nchi, katika bajeti ya Taifa, katika kuzuia migogoro na migomo, tumwambie Bwana shuka uingilie kati, naye atafanya! Tukatae kushindwa na kuona kwamba tumeshindwa,” alisisitiza.

Aliwataka waumini wote waache uvivu wa kuliombea Taifa. “Kila mmoja ana wajibu wa kuliombea Taifa hili na kuziombea familia zetu. Tusipoomba na Taifa likiingia katika vurugu nasi pia tutaathirika, kwa hiyo tunapaswa kulibeba Taifa hili katika maombi,” alisisitiza.

Akishukuru kwa maadhimisho ya siku ya akinamama wa kanisa la TAG, Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Mwenge TAG, Mch. Meshack Mhini alisema wanawake ni jeshi kubwa na akinababa hawana budi kutambua nafasi ya wanawake katika utumishi wa kanisa la leo.