WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amemteua Juma Shabani Mgoo (51) kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (Chief Executive Officer) wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services Agency – TFS).
Waziri amefanya uteuzi huo kwa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Wakala wa Serikali Sura Na. 245, kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Wakala wa Serikali mwaka 2009.
Kabla ya uteuzi huo Juma Mgoo alikuwa akitumikia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kama Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali Misitu na Ufugaji Nyuki (Ag. Director of Resources Management). Aidha, kabla ya Wakala wa Huduma za Misitu kuanza Juma Mgoo alikuwa akifanya kazi Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji Misitu.
Juma Mgoo ambaye ni mtaalam wa Misitu alihitimu Shahada ya Kwanza ya Misitu (BSc Forestry) katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 1986. Baadaye alihitimu Shahada ya Uzamili ya Uendelezaji wa Maliasili (MSc Natural Resources Management) katika Chuo Kikuu cha Norway mwaka 1992. Pia alihitimu masomo ya juu ya Ujasiriamali (Post Gradute Diploma in Entreprenuership and Enterprise Development) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2006.
Juma Mgoo ameitumikia Serikali katika vituo mbalimbali, pamoja na Songea kama Afisa Misitu na Kigoma kama Afisa Misitu Mkoa wa Miradi ya Misitu. Pia alifanya kazi Makao Mkuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Meneja Mradi wa Misitu ya Hifadhi na Mikoko, Mratibu wa Programu Taifa ya Misitu na Ufugaji Nyuki Tanzania (NFBKP), Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Maliasili (Management of Natural Resources Programme – MNRP) na Kiongozi wa Kamati ya Kuandaa Uanzishwaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ulianzishwa kisheria tarehe 1 Julai 2010, na kuanza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2011. Wakala huo umechukua shughuli za kiutendaji ambazo zilikuwa zinatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Uteuzi wa Juma Mgoo kama Ofisa Mtendaji Mkuu ni kuanzia tarehe 1 Desemba 2011 na utadumu kwa kipindi cha miaka mitano hadi tarehe 30 Novemba 2016.