Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHAHIDI wa 13 Gabriel Maleko katika kesi ya kupinga matokeo ya
uchaguzi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godless Lema (CHADEMA) ameieleza mahakama kuu kanda ya Arusha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilihusika katika kufungua shauri hilo.
Shahidi huyo ametoa madai hayo jana mahakamani hapo, na kudai kuwa
baada ya uchaguzi mkuu huyo CCM ilikutana katika kata ya Sokon I
kufanya tathmini ya matokeo ya uchaguzi mkuu huo wa mwaka 201o, ambapo pamoja na mambo mengine kiliazimia kufungua kei mahakamni kupinga ushindi wa Lema
Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Gabriel Rwakibarila, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa wajumbe wa kikao hicho waliazimia kufungua kesi baada ya kupata taarifa kuhusu maneno ya kashfa na udhalilishaji yaliyotolewa na Lema katika mikutano ya kampeni dhidi ya aliyekuwa mgombea kupitia CCM Dk. Batilda Burian.
Akihojiwa na wakili wa Serikali Timon Vitalis, shahidi huyo ambaye ni
balozi wa nyumba kumi na katibu mwenezi wa CCM, tawi la Sinoni alidai
kuwa kikao hicho kilihudhuriwa na mabalozi wa nyumba kumi na viongozi
mbalimbali ngazi ya tawi ambapo wawili kati yao walidai kushuhudia na
kusikia maneno hayo walijitolea kutoa ushahidi mahakamani iwapo kesi
itafunguliwa.
Alidai mahakamani hapo kuwa mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alikuwa ni Amina Ally ambaye alijitolea kutoa ushahidi na tayari ametoa shahidi mahakamani akiwa shahidi wa 11. Aidha madai ya shahidi huyo kuwa CCM imehusika kufungua kesi hiyo, amekuwa shahidi wa kwanza kutoa madai hayo ambapo mashahidi wengine wakiwemo wadai katika kesi hiyo wamekana mahakamani hapo kesi hiyo kuhusiana na CCM.
Awali akiongozwa na wakili wake, Alute Mughwai, shahidi huyo alidai
kumsikia Lema akiwaomba wananchi wasimchague Dk. Burian kwa sababu siyo mkazi wa jimbo la Arusha na uchaguzi utapokamilika angerejea Zanzibar alikoolewa kuhudumia familia yake.
Wakati akihojiwa na wakili, Method Kimomogoro anayemtetea Lema,
shahidi alidai kuwa baada ya kumsikia Lema akitoa maneno hayo dhidi ya Dk Buriana aliakwenda kutoa taarifa kwa katibu wa CCM kata ya Sokon I aliyemtaja kwa jina la Lameck Shosi kutekeleza maagizo na maelekezo ya chama hicho kwa wanachama wake iliyowataka kuhudhuria mikutano ya vyama vya upinzani na kutaarifu yanayozungumzwa na kutoka kwenye mikutano huo.