Kikwete awataka mawaziri waache ubabe, dhuluma, uzinzi

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja Mawaziri, Makatibu wakuu na viongozi waandamizi serikalini muda mfupi baada ya ufunguzi wa semina elekezi kwa viongozi wa umma inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha St. Gaspar mjini Dodoma. Wengine walioketi kutoka kushoto Waziri wa mabo ya ndani Shamsi Vuai Nahodha, Waziri mkuu mstaafu Cleopa David Msuya na Wziri mkuu Mizengo Pinda. Wengine ni Jaji Mkuu Othman Chande, Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, spika wastaafu Pius Msekwa na Samuel Sitta (picha na Freddy Maro)


Na Said Mwishehe
Dodoma

RAIS Jakaya Kikwete amewataka mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao katika Serikali yake kutotumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya dhuluma, wizi, ulevi, uzinzi, ubabe na udhalilishaji.

Amewataka watambue kuwa, hakuwateua kushika nafasi hizo kwa ajili ya kujifungua ofisini na kutazama TV, kusoma magazeti na kutumia muda mwingi kuangalia mtandao; bali kwa lengo moja la kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao.

Kikwete alisema hayo leo alipokuwa akifungua semina elekezi inayofanyika kwa siku nne kwa ajili ya mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wa wizara mjini Dodoma.

Alisema watumishi wa umma ambao wapo katika nafasi kubwa kama hizo wanapaswa kutambua kila wanachokifanya katika nafasi wanazotumikia ni kwa ajili ya wananchi na si kwa ajili yao ama kujinufaisha na kwamba wazingatiea maadili ya uongozi.

Alisema kuwa haitakuwa busara kuona nafasi walizonazo wanazitumia katika mambo ambayo hayaendeani na maadili ya uongozi na kutoa mfano kuwa waziri ama katibu mkuu wa wizara Fulani hapaswi kujihusisha na ubabe, uzinzi, uporaji,mla rushwa ,mnzizi ama mlevi.

“Haitakuwa vema kuona waziri ama naibu wake anakwenda baa anakunywa pombe hadi muda wa kufunga unapita akiaambia mzee muda umekwisha anajibu hunijui mi nani.Hapana viongozi wa umma na hasa ambao umepewa dhana ya kuongoza wizara mkazingatia maadili ya uongozi,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kitendo cha kutumika vibaya kwa nafasi za uongozi matokeo yake Serikali inaingia katika fedha kubwa ambayo haikutarajiwa bali imetokana na sababu za mtu mmoja tu na kuongeza haamini kama kuna mmoja wa mawaziri ama katibu wa wizara ambao wanajihusisha na mambo hayo bali amekumbusha tu mambo ambayo yanatakuwa kufanywa kwa ajili ya maslahi ya nchi.

Katika hili Rais kikwete alisisitiza umuhimu wa kiongozi kuwa mfano wa kuigwa hata na watumishi wengine katika eneo lake la kazi badala ya kuonekana ni kiongozi wa mfano mbaya na muda mwingi kutumika kunyooshewa vidole kwa mambo ya aibu anayoyafanya.

Rais Kikwete akiungumzia utendaji kazi wa Serikali yake li kufikia malengo ya kuwatumikia wananchi alisema kuwa, hakuna sababu ya viongozi hao wa wizara kwa maana ya waziri,naibu waziri, katibu mkuu na naibu katibu mkuu kukaa ofisini tu muda wote wakisoma magazeti, kuangalia mtandao ama kuangalia mafaili yaliyopo mezani bali wanatakiwa kwenda kwa wananchi.

Alisema alipofanya uteuzi hakuwa na lengo la kutaka viongozi hao wawe wanakaa ofisini bali anategemea kuona wakienda kwa wananchi na kupata ufumbuzi wa matatizo yaliyopo huko ambako wananchi wanakabiliwa na kero nyingi na hazina ufumbuzi.

Alisema kuwa ni lazima viongozi hao waende huko na kuongeza kuwa anashaa hivi sasa mawazri hawaendi kwa wananchi kuzungumza nao na kusikiliza matatizo yao hali hiyo inamshanaza na hajui sababu ni nini.

“Naomba mtoke mwende kwa wananchi ambao wana matatizo mengi tu lakini kuwepo kwenu ofisini yanakosa majibu. Inashangaza kuona kuona wamekaa kimya wala hazunguki kuangalia miradi. Makatibu wakuu na manaibu wao nao watoke ofisini.” Alisema JK.